'Siku ya Hussein (as)' yaadhimishwa mjini New York, bendera ya Hussein (as) yapepea
(last modified Mon, 09 Sep 2019 08:18:23 GMT )
Sep 09, 2019 08:18 UTC
  • 'Siku ya Hussein (as)' yaadhimishwa mjini New York, bendera ya Hussein (as) yapepea

Waislamu wa mji wa New York nchini Marekani kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo ya Iran, India, Pakistan na ya Kiafrika wamefanya maombolezo ya kukumbuka kifo cha Imam Hussein (as) mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw), katika mtaa wa Manhattan.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Redio na Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB, walioshiriki maombolezo hayo yaliyofanyika jana Jumapili, walipata fursa ya kuwabainishia Wamagharibi masaibu, mateso na mafundisho ya kuvutia aliyoyawasilisha Imam hussein (as) kupitia mapambano yake dhidi ya watawala dhalimu huko katika ardhi ya Karbala nchini Iraq.

Jumapili inayokaribia zaidi siku ya Ashura mjini New York imetangazwa kuwa ni "Siku ya Imam Hussein (as)'  au kwa jina jingine 'Hussein Day.'

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika maombolezo hayo ya Jumapili katika eneo la Manhattan, waombolezaji waliwapa wapita njia na waliokuwa karibu na maombolezo  hayo, ambao huenda ndio ilikuwa mara yao ya kwanza kusikia Imam Hussein (as) akitajwa, waridi nyekundu na vijikaratasi vya makaribisho, vilivyoandikwa maelezo kuhusiana na mapambano matakatifu ya mtukufu huyo katika jangwa la Karbala.

Maombolezo ya Imam Hussein (as) mjini Karbala, Iraq

Waombolezaji wa Imam Hussein (as) katika eneo la Manhattan kwa mara nyingine walitangaza kuwa jina la 'Hussein (as)' ni ngao ambayo kupitia kwake dini ya Mwenyezi Mungu ya Uislamu iliweza kubakia hai na kwamba wao ni wafuasi wa Imam ambaye ujumbe wake muhimu na wa kudumu milele ni, 'hatutakubali kudhalilishwa.'

Kwa mujibu wa takwimu, kuna Waislamu wa Kishia wasiopungua milioni mbili wanaoishi nchini Marekani.

Imam Hussein (as), ambaye ni Imam wa tatu wa Waislamu wa Shia, pamoja na wafuasi wake wachache watiifu, waliuawa shahidi na kwa njia ya kinyama tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijiria katika jangwa la Karbala nchini Iraq na mtawala dhalimu Yazid mwana wa Muawiyya.

 

Tags