Oct 13, 2019 02:24 UTC
  • Kutuma Pentagon wanajeshi na zana mpya za kijeshi nchini Saudi Arabia; harakati ya kimaonyesho

Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akidai kwamba anawaunga mono na kuwahami waitifaki wake katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Katika uwanja huo, Saudi Arabia ikiwa mshirika mkuu wa Washingtn katika eneo hili, ina nafasi maalumu katika siasa za kikanda za serikali ya Trump.

Kuhusiana na suala hilo, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) juzi Ijumaa Oktoba 11 ilitoa taarifa ikitangaza kuwa, nchi hiyo itatuma Saudia wanajeshi na zana zaidi za kivita. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanajeshi wapya 1800, mitambo miwili ya kurushia makombora ya Patriot, ngao moja ya ulinzi wa makombora aina ya TAD na squadroni mbili za ndege za kivita aina ya F-15 zitatumwa huko Saudia. Taarifa ya Pentagon imedai kuwa: Washington haitaki kuzidisha mivutano katika eneo la Asia Magharibi na kupigana vita na Iran, na kutumwa wanajeshi na zana hizo za kivita huko Saudia kimsingi kunafanyika kwa lengo la kudumisha mlingano na kutoa radiamali mkabala wa vitisho vinavyoweza kujitokeza. 

Ngao ya kujikinga na makombora ya Patriot

Hatua ya Pentagon ya kuatuma wanajeshi na zana mpya za kivita nchini Saudia imechukuliwa baada ya mashambulizi ya karibuni ya wanamapambano wa Yemen dhidi ya vituo vya mafuta vya shirika la mafuta la Saudia ARAMCO huko Abqaiq na Khurais mashariki mwa nchi hiyo, ambayo yalipelekea kupungua zaidi ya nusu ya uzalishaji mafuta wa Saudia. Kuwepo kwa mifumo na ngao za kujikinga na makombo nchini Saudi Arabia ukiwemo ule wa Patriot hususan kandokando ya taasisi muhimu za mafuta za nchi hiyo kama ile ya Abqaiq hakukuweza kuzuia ndege zisizo na rubani za wanamapambano wa Yemen kushambulia taasisi za mafuta za ARAMCO. Suala hilo limekabiliwa na ukosoaji mkubwa ndani na nje ya Saudi Arabia. Mwezi Septemba mwaka huu Pentagon ilituma wanajeshi 200 huko Saudi Arabia na mwezi huu wa Oktoba inatuma wengine 1000, suala linaloifanya idadi ya wanajeshi wa Marekani nchini humo kufikia 3000. Suala hilo pia limesisitizwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo ambaye ameandika katika ujumbe wake wa Twitter kwamba: "Marekani inatuma wanajeshi na zana zaidi za kivita nchini Saudi Arabia ili kuzidisha uwezo wa kiulinzi wa nchi hiyo."

Mike Pompeo na Mfalme Salman wa Saudia

Kama tulivyotangulia kusema, uamuzi wa Marekani wa kutuma wanajeshi na zama mpya za kivita huko Saudi umechukuliwa kwa kutiliwa maanani hali ya mvutano iliyopo katika Ghuba ya Uajemi na baada ya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Yemen dhidi ya taasisi muhimu zaidi za mafuta nchini humo. Baada tu ya mashambulizi hayo Washington ilielekeza kidole cha tuhuma kwa Tehran ikidai Iran imehusika na hujuma hiyo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekadhibisha tuhuma hizo na kuzitaja kuwa hazina msingi wana ushahidi wowote.

Marekani daima imekuwa ikiuunga mkono na kuukingia kifua utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, nchi ambayo inahesabiwa kuwa mshirika wa kistratijia na wa kiuchumi wa serikali ya Washington na mnunuzi mkubwa zaidi wa silaha kutoka Marekani. Kwa msingi huo, serikali ya Trump haitaki kabisa kuona uhusiano wake na Saudia ukiyumba au kuingia doa. Mbali na hayo, Donald Trump anaitumia Saudi Arabia kama wenzo wa kutimizia malengo yake na amekuwa akiudhalilisha na kuudunisha utawala huo wa Aal Saud kiasi cha kuwataja viongozi wake kuwa ni "ng'ombe mkamwa maziwa" wa Marekani. Kwa mfano tu baada ya mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya vituo vya mafuta vya Saudia, Donald Trump aliitaka Riyadh kuipatia fedha zaidi Marekani kwa ajili ya kuilinda na kuhami zaidi.

Kutumwa wanajeshi na zama mpya za kivita huko Saudi Arabia hususan ngao za kujikinga na makombora za Patriot na TAD na makumi ya ndege za kivita aina ya F-15 kwa hakika ni huduma ya kiusalama ya Washington kwa Saudia. Hapana shaka kuwa haduma hiyo haitatolewa bure bilashi, na Wasaudia watalazimishwa kuilipia gharama kubwa ya mabilioni ya dola.

Suala jingine la kusikitisha ni kuwa, hatua ya sasa ya Pentagon inaonesha kwamba, licha ya Saudi Arabia kununua silaha za mabilioni ya dola za Marekani kutoka Washington lakini Wasaudia hawawezi kuzitumia silaha hizo, na ununuzi wake hauwezi kuilinda nchi hiyo mbele ya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za wanapambano wa Yemen. Kwa msingi huo Riyadh imeamua kunyoosha mkono wa kuomba msaada kwa ajili ya kulinda usalama wake.       

Tags