Maelfu ya Waislamu waandamana Ufaransa kupinga chuki dhidi ya Uislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57203-maelfu_ya_waislamu_waandamana_ufaransa_kupinga_chuki_dhidi_ya_uislamu
Maelfu ya watu wameshiriki maandamano katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris kulalamikia chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 11, 2019 09:18 UTC
  • Maelfu ya Waislamu waandamana Ufaransa kupinga chuki dhidi ya Uislamu

Maelfu ya watu wameshiriki maandamano katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris kulalamikia chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo.

Vyombo vya habari vya Ufaransa vimeripoti kuwa, zaidi ya watu 13,000 walishiriki maandamano hayo ya jana Jumapili. Walioshiriki maandamano hayo wamesikika wakisema kuwa wanaunga mkono wanawake Waislamu wanaovaa niqabu, huku wengine wakipiga nara za kulaani ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu nchini humo.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji yalikuwa na jumbe zinazosema: "Tunapinga Chuki Dhidi ya Uislamu", na "Hapana kwa Chuki dhidi ya Waumini."

Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya Waislamu wawili kujeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi nje ya msikiti mmoja katika mji wa Bayonne, kusini magharibi mwa Ufaransa.

Maandamano ya kulaani chuki dhidi ya Uislamu mjini Paris

Shambulizi hilo dhidi ya msikiti lilifanyika wiki moja baada ya miji kadhaa ya Ufaransa ukiwemo mji mkuu Paris, Marseille, Lyon na Metz kushuhudia mikusanyiko mikubwa ya kulaani na kulalamikia ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu katika nchi hiyo ya Ulaya.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa wiki hii, asilimia 42 ya Waislamu nchini Ufaransa wameripoti kuwa wahanga wa vitendo vya ubaguzi wa kidini dhidi yao katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.