Indhari ya Mshauri wa Usalama wa Taifa Marekani kuhusu kusambaratika NATO
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57215-indhari_ya_mshauri_wa_usalama_wa_taifa_marekani_kuhusu_kusambaratika_nato
Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ni maarufu kwa kuibua utata, angali anaendelea kukosoa vikali Muungano wa Kijeshi wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO) . Trump hasa anawakosoa wanachama wa bara Ulaya katika muungano huo kwa kutotenga asilimia 2 ya Pato la Ndani la Nchi (GDP) kwa ajili ya gharama za kijeshi. Maafisa wa ngazi za juu wa Marekani nao sasa pia wanafuata nyayo za Trump katika kuukosoa muungano wa kijeshi wa NATO.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 12, 2019 07:57 UTC
  • Indhari ya Mshauri wa Usalama wa Taifa Marekani kuhusu kusambaratika NATO

Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ni maarufu kwa kuibua utata, angali anaendelea kukosoa vikali Muungano wa Kijeshi wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO) . Trump hasa anawakosoa wanachama wa bara Ulaya katika muungano huo kwa kutotenga asilimia 2 ya Pato la Ndani la Nchi (GDP) kwa ajili ya gharama za kijeshi. Maafisa wa ngazi za juu wa Marekani nao sasa pia wanafuata nyayo za Trump katika kuukosoa muungano wa kijeshi wa NATO.

Kuhusiana na hili,  Robert O'Brien Mshauri wa Usalama wa Taifa Marekani katika matamshi yenye msimamo mkali, amesema yamkini muungano wa kijeshi wa NATO ukasambaratika. Akizungumza Jumatatu Novemba 11 alisema: "NATO ni muungano muhimu kwetu lakini nadhani hitilafu ambazo zimeibuka katika muungano huu kutokana na kuwa nchi zilizo katika muungano huu hazitoi mchango wao kwa njia ya uadilifu kwa ajili ya kukidhi gharama za kijeshi." O'Brien ameongeza kuwa: "Kutokana na kuwa, Ujerumani na nchi zingine wanachama wa NATO hazitoi mchango wao wa kifedha kwa uadilifu, muungano huu unaelekea kusambaratika. Wameudhuru muungano huu hata zaidi ya hujuma ya hivi sasa ya Uturuki katika eneo la Kaskazini mwa Syria."

Pamoja na hayo, Mshauri wa Usalama wa Taifa Marekani amedai kuwa, Marekani ingali inafungamana na ahadi zake katika muungano huo wa miaka 70.

Ukosoaji wa O'Brien zaidi umelenga wanachama wa  NATO ambao hawatoi mchango wa kifedha unaotakikana kwa muungano huo. Inatazamiwa kuwa matamshi hayo ya wakuu wa Marekani yatajadiliwa katika kikao kijacho cha nchi wanachama wa NATO ambacho kimepangwa kufanyika mjini London.

Trump na maafisa wa ngazi za juu wa kisiasa na kijeshi katika utawala wake, katika mikutano na maafisa wa ngazi za juu pamoja na viongozi wa Ulaya, na pia katika vikao vya NATO, wamekuwa wakisisitiza kuhusu kushiriki zaidi nchi za Ulaya katika kuchangia bajeti ya NATO. Aidha wamewataka kutenga asilimia 2 ya Pato la Ndani la Nchi (GDP) kwa ajili ya gharama za kijeshi.

Trump katika mkutano wa NATO mnamo Julai 2018

Baada ya kuingia madarakani, Trump aliutaja muungano wa NATO kuwa uliochakaa na ambao unaigharimu Marekani kiasi kikubwa cha fedha. Trump aidha amechukua maamuzi ya upande mmoja bila kushauriana na wanachama wengine wa NATO, nukata hii inaashiria upuuzaji au dharau kwa waitifaki katika muungano huo.

Aghalabu ya wanachama wa NATO sasa wamebaini kuwa Trump ana mtazamo hasi kuhusu muungano huo wa kijeshi. Katika matamshi ambayo hayajawahi kuhushudiwa, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa  alisema shirika la kijeshi la NATO limekufa ubongo. Macron aliashiria maamuzi ya upande mmoja ya Marekani na Uturuki kaskazini mwa Syria ambapo Marekani iliondoa askari wake eneo hilo nayo Uturuki ikalivamia eneo hilo hilo na kusema hatua ya nchi hizo mbili zimetia dosari kubwa falsafa ya uwepo wa NATO.

Msimamo huo wa Macron umekosolewa vikali na Ujerumani ambayo ni moja kati ya wanachama muhimu wa Umoja wa Ulaya na NATO. Heiko Mass, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani ametoa tahadhari kwa Ufaransa kuhusu kuvuruga muungano wa NATO. Katika makala aliyoandika katika gazeti la kila wiki la Der Spiegel, Mass amesema kuuharibu Muungano wa Kijeshi  wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO) ni kosa. Alidai kuwa, bila Marekani, Ujerumani na Ulaya haziwezi kujilinda.

Pamoja na hayo, serikali ya Ujerumani ndiyo ambayo imekuwa ikikosolewa zaidi na Marekani kuhusu NATO. Wakuu wa Washington wanailaumu, Berlin kuwa haijatekeleza ahadi zake katika kugharamia bajeti ya NATO hasa kutenga asilimia 2 ya Pato la Ndani la Nchi (GDP) kwa ajili ya gharama za kijeshi.

Rais Macron wa Ufaransa

Matamshi makali ya Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani si tu kuwa ni onyo kali kwa Ujeurmani ambayo inasema Ulaya haiwezi kujilinda bila Marekani, bali pia ni kejeli kwa Macron ambaye amesema hatua za Marekani na Uturuki huko kaskazini mwa Syria ni sawa na kudhoofisha NATO.

Takwa la utawala wa Trump kwa wanachama wa NATO barani Ulaya ni kuwa, wasikilize na kutii amri zinazotoka Washington. Trump anatizama kila kitu kwa matazamo wa maslahi ya kibiashara na anaamini kuwa, iwapo NATO haitakuwa na faidha za kifedha kwa Marekani, basi uwepo wake katika muungano huo hautakuwa na faida na ni sawa na kupoteza pesa.