Umri wa kuishi Wamarekani unazidi kupungua
Matokeo ya uchunguzi mpya wa jarida la wiki la Newsweek la nchini Marekani unaonyesha kwamba umri wa kuishi Wamarekani unaendelea kupungua.
Matokeo hayo yamezidi kubainisha kwamba umri wa kuishi Wamarekani ambao wako katika umri wa kufanya kazi, umezidi kupungua kutokana na matumizi makubwa ya madawa ya kulevya, kujiua na magonjwa mbalimbali na kwamba mwenendo huo wa kupungua umri wa kuishi ulianza mwaka 2014. Kwa mujibu wa matokeo hayo, ongezeko la vifo kabla ya umri wa miaka 65 nalo limezidi kuongezeka na kwamba vifo zaidi vinawapata watu walio na umri wa kati ya miaka 25 hadi 65 takwimu ambazo zimesajiliwa zaidi katika maeneo kama vile ya Bonde la Ohio na Ukanda wa Dhahabu
Hii ni katika hali ambayo kwa miongo kadhaa maeneo hayo yamekuwa yakikabiliwa na mashinikizo ya kiuchumi na kijamii yanayotokana na kufungwa kwa viwanda vya madini ya mawe au viwanda vya aluminiamu na masuala tofauti ya usalama wa kiuchumi na ongezeko la kukosekana kwa fursa za kazi. Ukanda wa Dhahabu unaanzia jimbo la New York na Pennsylvania, Virginia Magharibi, Ohio, Indiana na Michigan na kuishia jimbo la Illinois na mashariki mwa Wisconsin. Maeneo hayo hapo kabla yalijulikana kwa jina la moyo wa viwanda wa Marekani. Matokeo hayo yametolewa katika hali ambayo Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akijitapa kwamba katika kipindi cha uongozi wake hali ya maisha nchini humo imezidi kuboreka kwa raia wake.