Mwanachama wa Republican nchini Marekani ataka Ilhan Omar anyongwe
Shirika la mtandao wa kijamii wa Twitter limelazimika kufuta akaunti za mgombea wa ubunge wa chama tawala cha Republican nchini Marekani, Danielle Stella kwa kuandika maneno ya kichochezi na kibaguzi dhidi ya Ilhan Omar, mbunge Muislamu katika Kongresi ya Marekani.
Mwanasiasa huyo wa chama cha Rais Donald Trump alitumia kurasa zake binafsi na za kampeni za Twitter kumshambulia na hata kutoa mwito wa kutaka kunyongwa Omar, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa sera za utawala wa Trump.
Mgombea huyo wa ubunge wa chama tawala nchini Marekani aliandika kwenye kurasa zake hizo maneno makali yanayosema: Ilham Omar anapaswa kushtakiwa kwa uhaini na kunyongwa.
Licha ya akaunti zake kufungwa na Twitter, lakini binafsi anashikilia kuwa hatua yake hiyo ni uhuru wa kujieleza, na alichofanya alitoa tu mwito wa kutekelezwa sheria ya uhaini dhidi ya mwanasiasa huyo wa chama cha upinzani cha Democratic. Hii si mara ya kwanza kwa mwanasiasa huyo wa Democrats kurushiwa maneno ya chuki, dharau, kejeli na vitisho.
Aprili mwaka huu, Polisi ya Upelelezi ya Marekani (FBI) ilimkamata na kumfungulia mashitaka Patrick Carlineo Junior mkazi wa mji wa New York, ambaye Machi 21 alimpigia simu mfanyakazi wa Ihan Omar, akitishia kuwa atamuua mbunge huyo mwenye asili ya Kisomali.
Ilhan Omar amekuwa akishambuliwa kila uchao kwa maneno makali ya chuki na ubaguzi na Trump pamoja na wafuasi wake wenye misimamo ya mrengo wa kulia.