Ripoti: Watoto walioko katika jela nchini Marekani wanabakwa na kudhalilishwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57837-ripoti_watoto_walioko_katika_jela_nchini_marekani_wanabakwa_na_kudhalilishwa
Ripoti mpya ya Taasisi ya Takwimu za Sheria ya Marekani imefichua kuwa, asilimia 7.1 ya watoto walioko katika mamia ya jela na vituo vya kurekebisha tabia vya watoto nchini Marekani walibakwa na kufanyiwa vitendo vingine vya udhalilishaji katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 12, 2019 21:13 UTC
  • Ripoti: Watoto walioko katika jela nchini Marekani wanabakwa na kudhalilishwa

Ripoti mpya ya Taasisi ya Takwimu za Sheria ya Marekani imefichua kuwa, asilimia 7.1 ya watoto walioko katika mamia ya jela na vituo vya kurekebisha tabia vya watoto nchini Marekani walibakwa na kufanyiwa vitendo vingine vya udhalilishaji katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Ripoti hiyo imesema watoto hao ama walibakwa au kuguswa sehemu zao za siri bila ridhaa zao, huku wengine wakionyeshwa picha na video chafu za ngono na maafisa au wafanyakazi wanaohudumu katika jela hizo. Watoto 6,000 walihusishwa kwenye uchunguzi huo uliofanywa katika jela na vituo 330 vya kurekebisha tabia za watoto nchini Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 26 ya watoto walifanyiwa udhalilishaji wa kingono ndani ya miezi 12 iliyopita katika kituo cha kutibu na kurekekbisha tabia za watoto cha Liberty Juvenile Unit for Specialized Treatment jimboni Florida.

Ripoti hiyo ya Taasisi ya Takwimu za Sheria ya Marekani imebainisha kuwa, vitendo hivyo vya watoto kubakwa na kudhalilishwa wakiwa jela na vituo vingine vya kuwazuilia vimeshamiri zaidi katika majimbo ya Florida na Texas, yakifuatiwa na majimbo ya Oregon, Arkansas, Idaho, Georgia, Ohio na New Jersey.

Maelfu ya watoto wananajisiwa katika jela za Marekani

Lovisa Stannow, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kutetea haki za wafungwa la Just Detention International amesema, "Kuripotiwa japo kisa kimoja cha udhalilishaji wa kingoni ni nyingi sana na ripoti hiyo inaonesha wazi kuwa, vitendo hivyo vinaendelea kuonekana kuwa vya kawaida katika vituo hivyo vinavayopaswa kuwa kimbilio na sehemu ya kurekebisha tabia za watoto hao nchini Marekani."

Naye Marsha Levick, afisa mkuu wa sheria katika Kituo cha Sheria za Watoto nchini humo amesema, "Kwa kuwa tumewatoa watoto hawa majumbani kwao, tuna wajibu wa kuwadhaminia usalama wao. Tunawatoa kwao tukidai kuwa tutawapa matibabu na kurekebisha tabia zao, lakini iwapo wanaandamwa na vitendo vya udhalilishaji wa kingono katika vituo hivi, basi tutakuwa tumewafelisha."