Apr 17, 2020 04:25 UTC
  • Makumi ya Waislamu wa Rohingya wafa kwa njaa ndani ya boti

Makumi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wamepoteza maisha kutokana na njaa baada ya boti yao kukwama baharini kwa majuma kadhaa.

Gadi ya Pwani ya Bangladesh ilisema jana Alkhamisi kuwa, boti hiyo iliyokuwa ikielekea Malaysia, ilikwama na kuelea katikati ya bahari kwa muda wa miezi miwili na ilifika kwenye ufuo wa bahari siku ya Jumatano baada ya kusukumwa na mawimbi.

Taarifa ya Gadi ya Pwani ya Bangladesh imesema zaidi ya Warohingya 24 wamepoteza maisha katika tukio hilo, lakini 382 walionusurika watarejeshwa Myanmar, walikokimbia mauaji na ukatili wa maafisa usalama wakishirikiana na Mabudha wenye misimamo ya kuchupa mipaka.

Februari mwaka huu, Waislamu 16 wa jamii ya Rohingya walifariki dunia baada ya boti yao kuzama katika Pwani ya Bengal, kaskazini mwa Bangladesh.

Ukatili dhidi ya Waislamu wa Rohingya ulianza tokea mwaka 2012

Waislamu wa Myanmar wanaume kwa wanawake pamoja na watoto wadogo wamekuwa wakifariki dunia mara kwa mara katika matukio ya kuzama boti wakikimbia mauaji na ukandamizaji unaofanywa na wanajeshi wa serikali ya Myanmar dhidi ya jamii hiyo.

Itakumbukwa kuwa wimbi jipya la mauaji, mashambulizi na ubakaji wa jeshi la Myanmar katika mkoa wa Rakhine kuwalenga Waislamu wa Rohingya, lilianza tarehe 25 Agosti mwaka 2017 ambapo zaidi ya Waislamu elfu sita waliuawa na wengine elfu nane kujeruhiwa. Aidha zaidi ya Waislamu wengine milioni moja wa jamii hiyo walilazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh.

 

Tags