Wamarekani wazidi kutwangana risasi wakati wa corona, mauaji yaongezeka kwa asilimia 200 New York pekee
(last modified Mon, 18 May 2020 00:40:58 GMT )
May 18, 2020 00:40 UTC
  • Wamarekani wazidi kutwangana risasi wakati wa corona, mauaji yaongezeka kwa asilimia 200 New York pekee

Ingawa kuna uchujaji mkubwa wa habari lakini pamoja na hayo, takwimu zilizotolewa na jeshi la polisi mjini New York Marekani zinaonesha kuwa, kesi za watu kupigana risasi wakati huu wa corona zimeongezeka sana, kiasi kwamba katika kipindi cha wiki moja tu iliyopita, kesi hizo ziliongezeka mara tatu zaidi ikilinganishwa na mwaka jana.

Toleo la mtandaoni la gazeti la New York Post limetangaza habari hiyo likinukuu ripoti ya jeshi la polisi wa mji wa New York likitangaza kwamba idadi ya kesi za watu kutwangana risasi mjini humo zimeongezeka mara tatu sawa na asilimia 200 ikilinganishwa na mwaka jana na hizo ni zile kesi tu zilizopripotiwa polisi.

Jeshi hilo la polisi limesema, katika kipindi cha wiki moja, watu 29 wameuawa kwa kupigwa risasi mjini humo na kwamba watu watano waliuawa siku ya Jumamosi pekee katika tena kipindi cha masaa mawili tu. Watu wengine saba waliripotiwa kupigwa risasi Jumamosi usiku, yaani siku hiyo hiyo waliyouliwa watu watano katika kipindi cha masaa mawili.

Mauaji ya kiholela ni jambo la kawaida sana nchini Marekani

 

Kwa upande wake, mchunguzi wa zamani wa kesi za jinai katika jeshi la polisi la New York, Joseph Giacalone amesema, watu wengi wako mabarabarani huku amri ya kutotoka nje iliyowekwa kama sehemu ya kupoambana na corona ikizidi kuvunjwa hivyo wahalifu nao wamerejea mitaani. 

Ongezeko kubwa la watu kupigana risasi huko Marekani linachangiwa na mambo mengi ikiwemo uhuru wa kumiliki na kutembea na silaha. Watu wengi wanauawa na kujeruhiwa kila siku lakini mashirika na magenge yanayounga mkono utengenezaji silaha hayaruhusu kupasishwa sheria za kupiga marufuku umiliki wa silaha kiholela nchini humo. Silaha zinauzwa kama bidhaa nyinginezo za kawaida madukani huko Marekani.

Maduka ya silaha yameenea kila sehemu nchini Marekani
Kununua na kumiliki silaha ni jambo rahisi sana huko Marekani

 

Tags