Guterres: Uingiliaji wa kigeni wa hivi sasa Libya haujawahi kushuhudiwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i62097-guterres_uingiliaji_wa_kigeni_wa_hivi_sasa_libya_haujawahi_kushuhudiwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema uingiliaji wa madola ya kigeni katika mgogoro wa Libya unaoshuhudiwa hivi sasa upo katika kiwango ambacho hakijawahi kuonekana tena huko nyuma.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jul 09, 2020 10:55 UTC
  • Guterres: Uingiliaji wa kigeni wa hivi sasa Libya haujawahi kushuhudiwa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema uingiliaji wa madola ya kigeni katika mgogoro wa Libya unaoshuhudiwa hivi sasa upo katika kiwango ambacho hakijawahi kuonekana tena huko nyuma.

Antonio Guterres amesema hayo katika hotuba yake kwa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika kwa njia ya intaneti na kuongeza kuwa, "mgogoro wa Libya umeingia katika marhala mpya, huku uingiliaji wa madola ya kigeni ukifikia kiwango cha kushtusha."

Amesema mbali na kupelekwa silaha nzito katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, lakini pia mamluki wa kigeni wanatumika katika vita vinavyoshuhudiwa hivi sasa nchini humo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasisitiza kuwa, kitendo cha kutuma mamluki na silaha nchini Libya kinakiuka moja kwa moja marufuku na vikwazo vya umoja huo.

Vita vya niaba vimeendelea kuyumbisha uthabiti nchini Libya

Mapigano ya ndani nchini Libya yameshtadi katika siku za karibuni kati ya wanajeshi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Waziri Mkuu, Fayez al-Sarraj na wanamgambo wanaoongozwa na Jenerali muasi Khalifa Haftar.  

Itakumbukwa kuwa, Uturuki inaiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya huku Misri, Imarati, Saudi Arabia, Jordan, Ufaransa na Russia zikimuunga mkono Jenerali Khalifa Haftar anayepigania kudhibiti mji mkuu Tripoli.