OIC yasikitishwa na maafisa wa Ufaransa kumtusi Mtume Muhammad (SAW)
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeeleza kusikitishwa kwake na hatua ya maafisa wa serikali ya Ufaransa ya kuendelea kumtusi na kumvunjia heshima Mtume Muhammad (SAW).
Taarifa iliyotolewa jana usiku na OIC imesema, kitendo cha baadhi ya vyombo vya habari na maafisa wa serikali ya Ufaransa cha kumvunjia heshima Mtume wa Uislamu hakitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuharibu na kutia doa uhusiano wa Paris na nchi za Kiislamu duniani.
OIC imesema wimbi la vitendo vya kumvunjia heshima Mtume Mtukufu linaloshuhudiwa Ufaransa kwa uungaji mkono wa maafisa wa serikali ya nchi hiyo ya Ulaya linazidi kupanda mbegu za chuki za kidini miongoni mwa Wafaransa.
Taarifa ya OIC imeongeza kuwa, vitendo vya namna hii vya kumvunjia heshima Mtume Muhammad (SAW) na matukufu ya kidini havitakuwa na matokea mengine ghairi ya kuvuruga jitihada za kimataifa za kukabiliana na chuki na misimamo mikali ya kufurutu ada.
Ufaransa ambayo ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya jamii ya Waislamu barani Ulaya, imekuwa ikishuhudia wimbi kubwa la hujuma na vitendo vya chuki na udhalilishaji dhidi ya Uislamu kwa lengo la kuharibu jina la dini hiyo na Mtume Muhammad (SAW).
Mwezi uliopita wa Septemba, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitetea kitendo cha jarida la nchi hiyo la Charlie Hebdo cha kuchapisha tena vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu akisema kuwa ni 'uhuru wa kusema na kujieleza'.