Rais wa zamani wa Ufaransa: Si sahihi kuwahusisha magaidi na Uislamu
Rais wa zamani wa Ufaransa, François Hollande amemuonya rais wa hivi sasa nchi hiyo Emmanuel Macron na kusema kuwa hapaswi kuwahusisha magaidi na dini ya Uislamu.
Shirika la habari la Anadolu limemnukuu rais huyo wa zamani wa Ufaransa akisema hayo wakati alipoonesha hisia zake kufuatia tukio la kigaidi la siku ya Alkhamisi lililotokea katika mji wa Nice nchini humo na kusisitiza kuwa, magaidi wanataka kuzusha vita vya kidini, hivyo si sahihi kuwahusisha Waislamu na magaidi hao.
Alkhamisi asubuhi, mtu mmoja alitumia silaha baridi kushambulia watu kadhaa mjini Nice Ufaransa na kuua watu watatu.
Alkahmisi hiyo hiyo, jeshi la polisi la Ufaransa lilitangaza kwamba limempiga risasi na kumuua mtu mmoja katika mji wa Avignon, wa kusini mashariki mwa nchi hiyo.
Mashambulizi ya silaha baridi yameongezeka katika siku za hivi karibuni huko Ufaransa ambapo matamshi ya kichochezi ya rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron yamechangia kuongezeka vitendo hivyo.
Rais huyo wa Ufaransa aliunga mkono jinai ya mwalimu mmoja wa Ufaransa ya kuwaonesha wanafunzi vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW kiasi kwamba hata alimpa nishani ya ushujaa mwalimu huyo baada ya kuuliwa na mtu mmoja mwenye hasira.
Nchi za Kiislamu zimelaani vikali uchochezi huo wa rais wa Ufaransa. Maandamano makubwa yanaendelea kufanyika katika ulimwengu wa Kiislamu kulaani uchochezi huo wa Emmanuel Macron.