Wapakistan: Hatutositisha maandamano mpaka balozi wa Ufaransa atimuliwe
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64653-wapakistan_hatutositisha_maandamano_mpaka_balozi_wa_ufaransa_atimuliwe
Maelfu ya waandamanaji nchini Pakistan waliofanya mgomo wa kuketi wametangaza kuwa wataendeleza mgomo wao huo mpaka balozi wa Ufaransa nchini humo atimuliwe.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Nov 16, 2020 03:41 UTC
  • Wapakistan: Hatutositisha maandamano mpaka balozi wa Ufaransa atimuliwe

Maelfu ya waandamanaji nchini Pakistan waliofanya mgomo wa kuketi wametangaza kuwa wataendeleza mgomo wao huo mpaka balozi wa Ufaransa nchini humo atimuliwe.

Maelfu ya wanaharakati wa kidini na waungaji mkono wa kundi la kidini liitwalo 'Vuguvugu la Labbayka' ambao walianzisha maandamano dhidi ya Ufaransa kutoka makao makuu ya mji wa Rawalpindi wakiwa na lengo la kusonga mbele hadi mji mkuu wa Pakistan, Islamabad wamekabiliwa na kizuizi cha vikosi vya jeshi la polisi.

Sambamba na kufanyika maandamano hayo, Shura Kuu ya kundi la Vuguvugu la Labbayka, imetangaza kuwa, serikali ya Pakistan inapaswa, mbali na kumfukuza balozi wa Ufaransa, imrejeshe nyumbani pia balozi wake aliyeko Paris na kuvunja mikataba yote ya kibiashara na kiuchumi iliyopo kati ya Pakistan na Ufaransa.

Umati wa waandamanaji waliozuiliwa na polisi

Wimbi jipya la maandamano dhidi ya Ufaransa linashuhudiwa katika miji mbalimbali ya Pakistan wakati mnamo wiki za karibuni, serikali ya Islamabad ilimwita balozi wa Ufaransa katika wizara ya mambo ya nje na kumtaka afikishe kwa serikali yake salamu za malalamiko makali ya Pakistan dhidi ya misimamo ya kupiga vita Uislamu iliyoonyeshwa na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na kuendelezwa kitendo cha kifidhuli cha jarida la Charlie Hebdo cha kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW.

Mnamo tarehe 15 Oktoba, Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan alisema, misimamo ya rais wa Ufaransa kuhusiana na kuchapishwa katuni zinazomvunjia heshima Mtume SAW imeziumiza hisia za Waislamu duniani na akasisitiza kwamba matamshi aliyotoa Macron yatashadidisha hisia za chuki dhidi ya Uislamu na kutoa fursa ya kutumiwa vibaya suala hilo na watu wenye misimamo ya kufurutu mpaka.../