Pakistan: Kamwe hatukubali kushinikizwa kuitambua rasmi Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64685-pakistan_kamwe_hatukubali_kushinikizwa_kuitambua_rasmi_israel
Kwa mara nyingine tena, Pakistan imesisitiza kuwa katu haitatumbukia katika mashinikizo ya kufuata mkumbo wa kuitambua rasmi Israel maadamu utawala huo haramu bado unazikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Nov 17, 2020 22:53 UTC
  • Pakistan: Kamwe hatukubali kushinikizwa kuitambua rasmi Israel

Kwa mara nyingine tena, Pakistan imesisitiza kuwa katu haitatumbukia katika mashinikizo ya kufuata mkumbo wa kuitambua rasmi Israel maadamu utawala huo haramu bado unazikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imekadhibisha madai ya baadhi ya vyombo vya habari vilivyodai kuwa, serikali ya Islamabad kupitia Waziri Mkuu wake, Imran Khan ipo chini ya mashinikizo makubwa ya Marekani ya kuitaka ianzishe uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.

Taarifa hiyo imekanusha habari hizo za uvumi zilizochapishwa na tovuti ya habari ya Middle East Eye na kueleza bayana kuwa, msimamo wa Pakistan kuhusu kadhia ya Palestina uko wazi na wala hautabadilika.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imesema suluhu yoyote ya kadhia ya Palestina sharti iungwe mkono na ikubaliwe kikamilifu na Wapalestina wenyewe.  

Wapakistani katika maandamano ya kupinga Muamala wa Karne

Huko nyuma pia, Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan binafsi alisema kuwa nchi yake kamwe haitautambua rasmi utawala haramu wa Israel.

Alisisitiza kuwa, msimamo huo unaoana na agizo lililotolewa na mwasisi wa Pakistan, Muhammad Ali Jinnah wa kulitetea taifa la Palestina mkabala wa utawala wa Kizayuni wa Israel; na  kwamba Waislamu wanapaswa kuwajibika mbele ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na kadhia ya Palestina.