Zarif: Usalama haupatikani kwa kuvuruga usalama wa wengine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema usalama na maslahi hayapatikani mkabala wa kuvuruga usalama na kutozingatia maslahi ya wengine.
Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran amebainisha hayo katika makala aliyoandika kaitka gazeti la Italia la La Republica chini ya anwani ya "Msimu Mpya ya Ushirikiano wa Iran na Ualya". Katika makala hiyo iliyoandikwa kwa munasaba wa safari ya hivi karibuni ya Rais wa Iran Ufaransa na Italia, Zarif amesema hakuna nchi inayoweza kudai kuwa inapambana na makundi ya kigaidi ya Al Qaeda na ISIS au Daesh katika hali ambayo imehusika katika kuenea makundi hayo nchini Yemen na Syria.
Zarif amesisitiza kuhusu udharura wa kustawisha ushirikiano baina ya Iran na Ulaya na kupambana na misimamo mikali ili usalama na utulivu urejee katika eneo. Aidha amesema nchi za Ulaya zinaweza kuzishawishi nchi za Mashariki ya Kati kutumia mazungumzo katika kutatua matatizo ya eneo.
Zarif amebainisha pia wasiwasi wa pamoja wa Iran na Ulaya kuhusu kuenea ugaidi Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa usalama na uthabiti ni hitajio la kimsingi la eneo la Mashariki ya Kati, Ulaya na dunia nzima.
Zarif amesema kuwa kupambana na umasikini, ukosefu wa uadilifu wa kiuchumi, kuhimiza demokrasia na kujizuia kuzusha hitilafu za kimadhehebu na kikabila na kupinga hatua za upande mmoja za kijeshi kuwa mbinu muafaka za kurejesha uthabiti Mashariki ya Kati.