Onyo la mashirika 4 ya Umoja wa Mataifa kuhusu hatari ya usalama wa chakula duniani
(last modified 2022-04-14T07:22:58+00:00 )
Apr 14, 2022 07:22 UTC
  • Onyo la mashirika 4 ya Umoja wa Mataifa kuhusu hatari ya usalama wa chakula duniani

Benki ya Dunia, Shirika la Biashara Duniani, Mfuko wa Fedha wa Kimataifa na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa zimeonya kuwa usalama wa chakula duniani uko hatarini na kwamba nchi zote zinapaswa kuchukua hatua maalumu kudhamini chakula kwa watu wao.

Tahadhari hiyo imetolewa kufuatia vita vinavyoendelea baina ya Russia na Ukraine, nchi mbili zenye mchango mkubwa katika uzalishaji wa ngano, nafaka na mbegu za mafuta duniani.

Katika wiki za hivi karibuni, bei ya baadhi ya vyakula katika masoko ya dunia imepanda kwa kasi, na baadhi ya nchi zimekabiliwa na mdororo wa kiuchumi au kusitishwa kwa uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje.

Shirika la habari la Iran, IRNA, limeripoti kuwa, mashirika hayo ya kimataifa yametoa taarifa yakizitaka nchi zote kujiepusha kupiga marufuku usafirishaji wa chakula na mbolea nje ya nchi na kuchukua hatua za haraka na za pamoja katika nyanja za usalama wa chakula.

Taarifa hiyo iliyotolewa jana Jumatano (tarehe 13 Aprili) ilisisitiza kwamba vita vya Ukraine vimeongeza mashinikizo yaliyosababishwa na mlipuko wa ugonjwa wa Corona, mabadiliko ya hali ya hewa na mivutano inaoongezeka ya kikanda, na kusababisha tishio kwa mamilioni ya watu ulimwenguni kote.

Taasisi hizo nne za kimataifa zinaonya katika taarifa yao ya pamoja kwamba, hali hii inazidisha mashinikizo kwa raia na ni tishio kubwa haswa kwa nchi masikini.

Shirika la Biashara Duniani (WTO) linatabiri kuwa nchi maskini ziko katika hatari kubwa zaidi kutokana na vita vya Ukraine kwa sababu zinatumia sehemu kubwa ya mapato yao kwa ajili ya chakula kuliko nchi tajiri.

Tags