Watetezi wa Palestina wafanya maandamano mbele ya ubalozi wa Israel mjini New York
(last modified 2022-04-22T01:52:01+00:00 )
Apr 22, 2022 01:52 UTC
  • Watetezi wa Palestina wafanya maandamano mbele ya ubalozi wa Israel mjini New York

Makundi ya wapinzani wa utawala ghasibu wa Israel yamefanya maandamano mbele ya ubalozi mdogo wa Tel Aviv mjini New York, Marekani na kutangaza uungaji mkono wao kwa wananchi madhulumu wa Palestina. Maandamano hayo yamefanyika kupinga ukatili na jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.

Waandamanaji hao waliojumuisha makundi yanayopinga Uzayuni kama Harakati ya Vijana wa Palestina, walipiga nara kama vile "Palestina itakombolewa kutoka kwenye mto hadi baharini". Vilevile wametoa wito wa kuendelezwa mapambano na utandawazi wa Intifadha ya Palestina.

Ripoti zinasema, nara na kaulimbiu zilizotolewa na waandamanaji hao mjini New York zimewatia wahka na kiwewe wabadiplomasia wa Israel. 

Msemaji wa ubalozi mdogo wa Israel katika mji huo amesema kuwa kaulimbiu na nara za waandamanaji hao zinatia wasiwasi. Mwanadiplomasia huyo amejaribu bila ya mafanikio kutetea dhulma na jinai za miongo kadhaa sasa za utawala huo dhidi ya watu wa Palestina na kudai kuwa, nara kama hizi ndizo zilizochochea machafuko ya wiki za karibuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Akieleza wasiwasi wake juu ya kupanuka zaidi Intifadha ya Wapalestina, afisa huyo wa utawala wa Kizayuni wa Israel amedai kuwa, baadhi ya watu wanataka kuleta machafuko hayo mjini New York!

Ijumaa iliyopita (15 Aprili) wanajeshi wa utawala haramu wa Israel waliwashambulia Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ndani ya Msikiti wa al Aqsa huko Quds inayokaliwa kwa mabavu na kujeruhi Wapalestina wasiopungua 160. Waislamu wengine zaidi ya 400 wametiwa nguvuni. Hujuma hiyo imezusha machafuko makubwa katika ardhi za Palestina inayokaliwa kwa mabavu. 

Tags