Oct 29, 2022 11:15 UTC
  • Ukosoaji mkali wa Putin kwa mauaji ya kigaidi ya shahidi Luteni Jenerali Soleimani

Akizungumza juzi Alhamisi katika Kongamano la Valdai, Rais Vladmir Putin wa Russia amekosoa mfumo na siasa za Magharibi na kueleza kuwa nchi za Magharibi zilimuua Luteni Jenerali Soleimani; katika hali ambayo shakhsia huyo alikuwa kiongozi rasmi nchini mwake na kuongeza kwamba Wamagharibi si tu hawajakana jambo hilo bali wanajifakharisha nalo.

Putin amesema: "Wao ndio walimuua Jenerali huyo wa Iran. Kulingana na mfumo wa sera za nchi za Magharibi, unaweza kumtendea Soleimani lolote unalotaka; ilhali huyo ni kiongozi rasmi wa nchi nyingine." Ameongeza kuwa: "Walimuua kiongozi huyo katika nchi ya tatu, na kujigamba kuwa 'ndio, sisi ndio tuliomuua." Haya yote ni kwa ajili ya nini? Tunaishi katika dunia gani?" 

Putin amekosoa vikali mauaji hayo ya kigaidi, kinyama na yaliyo kinyume cha sheria yaliyotekelezwa dhidi ya Luteni Jenerali  shahidi Solemani na wakati huo huo  kukosoa mfumo jumla wa kimataifa wa nchi za Magharibi ikiwemo Marekani ambazo huchukua kila hatua ambayo ina maslahi kwazo huku zikipuuza na kukanyaga sheria na kanuni za kimataifa ikiwemo hati ya Umoja wa Mataifa. Rais Putin katika uwanja huo ameashiria mfumo wa dunia unaoongozwa na Wamagaribi kwa jina la "Utaratibu Unaozingatia Sheria" na kusema: "hakuna anayejua  sheria hizo za kimataifa zilibuniwa na nani na pia zinayaruhusu madola yenye nguvu duniani kufanya lolote zinalotaka."  

Katika hatua yake ya kijinai, rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump alitoa amri ya kuuliwa kigaidi Luteni Jenerali Qassim Soleimani aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na wanajihadi wenzake wanane aliokuwa ameambatana nao. Luteni Jenerali Soleimani na Abu Mahdi al Muhandes Naibu Mkuu wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq cha Hashdu Shaabi pamoja na wenzao 8 waliokuwa pamoja nao waliuliwa shahidi alfajiri ya Januari 3 mwaka 2020 katika hujuma ya kigaidi ya anga ya wanajeshi vamizi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad mji mkuu wa Iraq. Marekani ilitekeleza jinai hiyo kwa madai kuwa Luteni Jenerali Soleimani alienda Iraq kwa lengo la kuratibu mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Marekani na kambi zao nchini humo na kuwa shambulio hilo la anga lilikuwa eti ni hatua ya kujilinda. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa ngazi za juu wa Iraq walipinga madai hayo ya Marekani. Adel Abdul Mahdi Waziri Mkuu wa Muda wa Iraq alisema tarehe 5 Januari mwaka 2020 katika kikao cha bunge la nchi hiyo kuwa, Luteni Jenerali Soleimani alikuwa ameingia Baghdad kwa minajili ya kuwasilisha ujumbe wa Iran kwenda Saudi Arabia.

Mashahidi Qassim Soleimani na Abu Mahdi al Muhandes 

Kwa utaratibu huo, madai ya uwongo ya Washington yamebainika wazi. Ni wazi kuwa, serikali ya Trump ilikuwa na azma ya kumuua Luteni Jeneraali Soleimani tokea mwaka 2018 na ilikuwa ikisubiri fursa muafaka ili kutekeleza jinai hiyo. Kwa mtazamo wa washauri wa kijeshi na kiusalama wa Trump ni kuwa, Marekani haikupasa kupoteza fursa  ya kuwepo kwa wakati mmoja Kamanda Soleimani na Abu Mahdi al Muhandes huko Baghdad ambao walihesabika kuwa makamanda wawili muhimu wa Iran na Iraq ambao walikuwa na mchango mkubwa katika vita dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh; na wakati huo huo wakitambulika kuwa miongoni mwa vizuizi vikuu vya kufikiwa malengo haramu ya Marekani katika Asia Magharibi, na kwa utaratibu huo Wamarekani wakatenda jinai hiyo kupitia hujuma ya kiuoga ya kigaidi dhidi ya makamanda hao.  

Jinai hiyo ya kinyama ya Marekani ilikabiliwa na radiamali na kulaani pakubwa kikanda na kimataifa. Bi Agnès Callamard Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na mauaji yaliyo kinyume cha sheria na ya kiholela katika Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa umoja huo mwaka jana alitaja kuuliwa shahidi Luteni Jenerali Qassim Soleimani kuwa kinyume cha sheria. Katika ripoti aliyotoa, Bi Callamard alipinga madai ya viongozi wa Marekani kuhusu sababu za kumuuwa kigaidi Luteni Jenerali Soleimani na kuandika: Washington imeshindwa kuwasilisha nyaraka na ushahidi wa kutosha ili kuhalilisha sababu ya kutenda hujuma hiyo. Callamard aliandika hivi kuhusu suala hilo: "Sababu iliyotolewa na Marekani ya kuhalalisha shambulio lake la droni dhidi ya Jenerali Soleimani haina mashikio yoyote kwamba kulikuwepo na tishio tarajiwa. Wanajeshi wa Marekani hawakukidhi vigezo viwili vya udharura na haja katika mauaji ya afisa wa Iran Jenerali Soleimani na mauaji hayo ya kigaidi yanakinzana na sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu."

Bi Agnes Callamard, Ripota Maalumu wa UN 

Rais Putin amezungumzia kwa mara nyingine tena mauaji ya kinyume cha sheria ya Luteni Jenerali shahidi Soleimani akikosoa pakubwa muamala jumla unaotekelezwa na Wamagharibi dhidi ya nchi nyingine duniani katika fremu ya mfumo wa kimataifa wa mabavu unaotawala dunia wa nchi hizo na hasa Marekani,  wa  kuhalalisha hatua zozote zinazokuwa kwa maslahi yao haramu. Hii ni katika hali ambayo nchi za Magharibi huziarifisha hatua na maamuzi yanayochukuliwa na nchi pinzani na adui zao kama hatua za kiuhasama na kigaidi.

Tags