Russia yakataa masharti ya Biden kukutana na Putin
https://parstoday.ir/sw/news/world-i91298-russia_yakataa_masharti_ya_biden_kukutana_na_putin
Siku ya Ijumaa, Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin, ilikataa sharti ambalo Rais wa Marekani Joe Biden alikuwa ameliweka kwa ajili ya mazungumzo na Vladimir Putin kuhusu mgogoro wa Ukraine na kutangaza kwamba mashambulizi ya Russia dhidi ya Ukraine yataendelea.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 04, 2022 06:09 UTC
  • Russia yakataa masharti ya Biden kukutana na Putin

Siku ya Ijumaa, Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin, ilikataa sharti ambalo Rais wa Marekani Joe Biden alikuwa ameliweka kwa ajili ya mazungumzo na Vladimir Putin kuhusu mgogoro wa Ukraine na kutangaza kwamba mashambulizi ya Russia dhidi ya Ukraine yataendelea.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari kwamba: "Rais Biden alisema kwamba mazungumzo yatawezekana tu wakati Putin atakapoondoa (majeshi yake) kutoka Ukraine." Moscow bila shaka haikubali masharti kama hayo. Ni kwa msingi huo ndio Peskov akatangaza kuendelea kwa "operesheni maalum za kijeshi za Russia huko Ukraine". Peskov hata hivyo amesisitiza kuwa Russia daima iko tayari kufanya mazungumzo.

Siku ya Alhamisi, wakati wa ziara rasmi ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron nchini Marekani, Joe Biden alitangaza kwamba ikiwa kweli Putin ana nia ya kumaliza mzozo wa Ukraine, atakuwa tayari kuzungumza na rais huyo wa Russiai. Pia aliongeza kuwa wamekubaliana na rais wa Ufaransa kumuwajibisha Putin kuhusu kuendeleza mzozo nchini Ukraine.

Msimamo mpya wa rais wa Marekani unaashiria mabadiliko ya kimsingi katika msimamo wake wa awali kuhusu vita vya Ukraine. Kwa kweli, Biden amegeuka kwa digrii 180 katika mtazamo wake wa hapo awali, aliposema mnamo Machi kwamba lazima Putin aondoke madarakakani. Biden alidai kuwa Putin alifanya hesabu mbaya kwa kuishambulia Ukraine na ikiwa yuko tayari kuondoa vikosi vyake nchini humo,  atakuwa tayari kukutana naye baada ya kushauriana na washirika wa Marekani katika NATO.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov

Sababu anuwai zinaweza kutajwa katika muktadha wa mabadikiko makubwa katika msimamo wa Biden. Kwanza, mafuriko ya misaada ya silaha kutoka Ulaya na Marekani kwenda Ukraine sasa yamepungua, hasa kutoka nchi za Ulaya. Kwa hakika, wanachama wa NATO wa Ulaya hawana hifadhi kubwa ya silaha kama Marekani, na kwa hiyo nchi hizo sasa zinazungumza kuhusu kupungua kwa maghala yao ya risasi na silaha na kutowezekana kuendelea kuzipeleka Ukraine.

Kuhusiana na hilo, siku ya Alhamisi, wabunge wa Italia walifuta mswada ulioiruhusu nchi hiyo kupeleka silaha Ukraine bila idhini ya bunge. Nchi nyingine za Ulaya, ikiwemo Ujerumani, zinakabiliwa na tatizo sawa na hilo. Kwa njia hiyo, Marekani italazimika taratibu kuwa mpelekaji pekee wa silaha huko Ukraine. Kwa kutilia maanani matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani ambapo  Warepublican walipata wingi wa viti katika Baraza la Wawakilishi, utawala wa Biden utakabiliwa na upinzani mkubwa wakati wa kuidhinisha bajeti inayohitajika kwa ajili ya kutuma silaha nchini Ukraine.

Warepublizan wanataka kupunguzwa na kuchunguzwa kwa karibu msaada  wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine. Tangu kuanza mzozo wa Ukraine, Marekani imeupa utawala wa Kyiv uungaji mkono mkubwa wa kifedha, kijeshi na kidiplomasia ambapo kufikia sasa imeipa Ukraine silaha zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 20. Hivi karibuni pia Bunge la Kongresi la Marekani liliidhinisha msaada wa dola bilioni 40 kwa Ukraine. Bila shaka lengo kuu la Marekani katika kujaribu kuendeleza vita nchini Ukraine ni kuiingiza Moscow katika vita vya muda mrefu, jambo ambalo litapelekea kudhoofika zaidi kwa nguvu za kijeshi na kupungua rasilimali za kifedha za Russia.

Ni kwa sababu hiyo ndio, Washington na mshirika wake wa Ulaya, Uingereza, hadi sasa zimetuma kiasi kikubwa zaidi cha msaada wa silaha kwa Kiev. Hata hivyo, itakuwa vigumu sana kuendeleza msaada huo katika siku zijazo. Bila shaka, Russia  inaamini kwamba ni  hatua za nchi za Magharibi na msaada wao mkubwa wa kifedha na silaha kwa Ukraine, ndio umeipelekea nchi hiyo kupinga kabisa pendekezo lolote la kufanyika mazungumzo ya kusitisha mapigano au kuanzisha mchakato wa amani na Russia.

Eneo la Donbass la Ukraine limejitangazia uhuru na kujiunga na Russia

Sababu nyingine ya Biden kubadilisha msimamo wake mkali wa hapo awali ni shinikizo la serikali za Ulaya ambazo zinataka kusitisha vita vya Ukraine kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii ya nchi za Ulaya. Katika kipindi cha utawala wa Biden na kuimarika muungano wa kijeshi wa NATO, serikali za Ulaya zimeiwezesha Marekani kupata satwa na ushawishi mkubwa barani humo, bila kujali matokeo mabaya ya kuendelea kwa hali hiyo dhidi ya Russia. Hali hii  imewakasirisha raia wa Ulaya wanaotaka kubadilishwa siasa za sasa na kuhitimishwa vita vya Ukraine.

Sababu nyingine ya kubadilika msimamo wa Biden ni kukatishwa tamaa Wamagharibi baada ya kubainika kuwa  jeshi la Ukraine haliwezi kupata ushindi katika vita vya sasa wala kukomboa maeneo yanayokaliwa na Russia ambayo sasa Moscow imeyataja kuwa ni sehemu ya ardhi yake.

Licha ya msaada mkubwa wa silaha kutoka Magharibi, Waukraine wamepiga hatua ndogo sana katika maeneo kama Kherson, na kwa kuingia majira ya baridi kali, hakutakuwa na harakati yoyote ya mafanikio kwenye medani ya vita ya Ukraine.