Makumi ya Waislamu wauawa katika shambulizi lililolenga msikiti Peshawar, Pakistan
(last modified Mon, 30 Jan 2023 12:37:24 GMT )
Jan 30, 2023 12:37 UTC
  • Makumi ya Waislamu wauawa katika shambulizi lililolenga msikiti Peshawar, Pakistan

Watu wasiopungua 56 wameuawa katika shambulizi la kujilipua kwa bomu lililotokea katika msikiti wa mji wa Peshawar huko kaskazini magharibi mwa Pakistan.

Vyombo vya usalama vya Pakistan vimeripoti kuwa, Waislamu wasopungua 56 wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika mlipuko kubwa uliotokea ndani ya msikiti wa mji wa Peshawar. 

Maafisa wa hospitali za mji huo wanasema idadi ya waliofariki dunia huwenda ikaongezeka kutokana na idadi kubwa ya majeruhi wa hujuma hiyo. 

Afisa wa polisi ya mji wa Peshawar, Sikandar Khan, aliambia shirika la habari la Reuters kwamba mlipuko huo umetokea wakati idadi kubwa ya Waislamu walipokuwa wamekusanyika kwa ajili ya ibada ya Swala. Khan ameongeza kuwa: "Sehemu moja ya jengo la msikiti huo imeanguka, na watu kadhaa wanaaminika kuwa chini ya vifusi vyake".

Image Caption

 

Maafisa wa usalama wanasema, gaidi aliyetekeleza hujuma hiyo alikuwa kwenye safu ya mbele wakati alipojilipua na kuwajeruhi makumi ya waumini waliokuwa wakitekeleza Swala ya Adhuhuri.

Mkuu wa polisi ya Peshawar, Muhammad Ijaz Khan, amesema katika taarifa yake kwenye televisheni ya Pakistan kwamba msikiti huo ulikuwa na uwezo wa kuwa na karibu watu 300 na ulikuwa umejaa wakati wa mlipuko huo.

Mwandishi wa televisheni ya Aljazeera ya Qatar nchini Pakistan amesema kundi la Taliban la Pakistani limedai kuhusika na shambulizi hilo katika ujumbe wa Twitter, ingawa mamlaka ya Pakistani haijatoa tamko lolote kuhusiana na suala hilo mpaka sasa.

Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif amelaani shambulizi hilo na kuamuru vyombo husika kuhakikisha matibabu bora zaidi yanatolewa kwa waathiriwa. Vilevile ameahidi kuchukua "hatua kali" dhidi ya wale waliohusika na shambulio hilo.