Mabudha wenye chuki washambulia msikiti wa Waislamu Myanmar
Katika kuendelea kwa maudhi dhidi ya jamii ya Waislamu nchini Myanmar, juzi usiku makumi ya Mabudha wenye misimamo mikali walishambulia msikiti mmoja katikati ya nchi hiyo na kuwaua Waislamu kadhaa waliokuwa msikitini hapo.
Kufuatia shambulio hilo, Waislamu walikimbilia kituo kimoja cha polisi kwa ajili ya kuokoa maisha yao. Shambulio hilo limejiri baada ya Mabudha wapatao 200 kuwashambulia Waislamu katika moja ya vijiji vya mkoa wa Bago. Shambulio hilo lilitekelezwa baada ya kujiri tofauti za kimaneno juu ya ujenzi wa shule moja ya Kiislamu katika eneo hilo. Afisa mmoja amesema kuwa, katika shambulio hilo lililofanywa usiku wa kuamkia leo, Mabudha hao wameharibu kabisa msikiti huo wa Waislamu. Kadhalika Mabudha hao wamefukua makaburi ya Waislamu na kuwalzimu karibu Waislamu wapatao 70 wakiwamo watoto wadogo walikimbilia kituo cha polisi kwa ajili ya kuokoa maisha yao. Waislamu wa mji huo wamesema kuwa, wana wasi wasi wa kurejea majumbani kwao kutokana na kuwepo uwezekano mkubwa wa Mabudha hao kuwashambulia ndani ya nyumba zao na kuwaua. Hii ni katika hali ambayo hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulitangaza habari ya kuendelea jinai za mabudha dhidi ya Waislamu nchini humo.