Mar 10, 2021 12:02 UTC
  • Ubaguzi wa rangi katika familia ya kifalme ya Uingereza

Licha ya madai ya nchi za Magharibi kuwa zinazingatia usawa wa watu katika jamii na kuheshimu haki za binadamu, lakini ukweli wa mambo ni kuwa nchi hizo zinatekeleza siasa za ubaguzi dhidi ya raia wao katika nyanja mbali mbali za kijamii na kiutamaduni.

Kuhusu hilo ufichuaji uliofanywa hivi karibuni na Megan Markle, bi harusi aliyeolewa katika familia ya kifalme ya Uingereza kwamba familia hiyo inahusika na ubaguzi wa rangi na uongo, ni dalili ya wazi kuhusu suala hilo. Megan na Mwanamfalme Harry ambao mwezi Januari walijivua rasmi majukumu yao ya kifalme na kuhamia Marekani, hivi karibuni walishiriki katika mahojiano ya televisheni ambapo walianika wazi mahusiano na siasa zinazoendeshwa katika familia ya kifalme ya Uingereza. Katika mahojiano hayo, Megan Markle alifichua kuwa wakati alipokuwa na ujauzito wa mwanae Archie, wasiwasi mkubwa iliokuwanao familia hiyo ni kuhusu kiwango cha weusi ambao angekuwa nao mtoto huyo na kwa msingi huo haikuwa tayari kumpa anwani na hadhi yoyote ya kifalme.

Hata kama hii ni mara ya kwanza kwa bi harusi katika familia ya kifalme ya Uingereza kuzungumzia rasmi ubaguzi unaofanyika katika familia hiyo lakini ripoti za kuwepo ubaguzi wa rangi nchini Uingereza na hasa katika ukoo wa kifalme wa nchi hiyo si jambo jipya. Ukoo huo ambao una utajiri na madaraka makubwa umeweka sheria maalumu ambazo zinapaswa kuzingatiwa. Moja ya sheria hizo ni kuwa wanawafalme wanapaswa kufuata sheria kali za ndoa na kuishi chini ya sheria hizo bila kuzikiuka. Pamoja na hayo baadhi ya wanafamilia hukiuka sheria hizo na kujiamulia kuishi maisha wanayoyapendelea wao. Mfano wa wazi katika uwanja huo ni katika zama za Edward wa VIII, mfalme wa wakati huo wa Uingereza ambaye aliamua kuweka pembeni taji la ufalme na kuamua kumuoa mwanamke mmoja aliyetalikiwa raia wa Marekani.

Kasri la ufalme wa Uingereza, Buckingham

Pamoja na kuwa katika miongo ya karibuni ufalme wa Uingereza umedai kufuta baadhi ya sheria za kale ambazo hazioani na mazingira ya ulimwengu wa sasa, lakini matukio yaliyojitokeza karibuni katika ndoa ya Megan Markle Mmarekani na mjukuu wa Malkia Elizabeth II, kwa mara nyingine tena yameanika wazi udhibiti wa sheria hizo za kale kwenye maisha binafsi ya wanawafalme wa Uingereza. Kwa kadiri kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na hasa baada ya Megan na Harry kuamua kuhamia Marekani, wajuzi wa mambo na wanaharakati wengi wamesema kwamba uamuzi huo ulitokana na tabia za kibaguzi na mashinikizo yaliyopo katika ukoo wa ufalme wa Uingereza. Kwa kadiri kwamba John Bercow, msemaji wa zamani wa bunge la Ungereza alisema kwamba: 'Ninaamini kuwa Megan amekuwa muhanga wa ubaguzi wa rangi wa moja kwa moja na matatizo mengine. Ni wazi kuwa amekabiliwa na ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa kijinsia na miamala mibaya.'

Ubaguzi wa rangi hauonekani tu katika kasri la ufalme wa Uingereza bali katika ngazi zote za jamii ya nchi hiyo. Mfano wa wazi kuhusu hilo ni kadhia ya Bi Rakhia Ismail, ambaye alikuwa meya wa kwanza Mwislamu kuvalia hijabu katika historia ya nchi hiyo, hatimaye alilazimika kujiuzulu kutoka chama cha Leba kutokana na ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu.

Ripoti zinazotolewa mara kwa mara kuhusu miamala ya ubaguzi wa rangi inayofanywa na polisi ya Uingereza na hasa dhidi ya raia weusi na jamii za wachche nchini humo ni dalili nyingine ya wazi katika uwanja huo. Kwa mujibu wa takwimu rasmi, idadi ya raia weusi na waafuasi wa dini za wachche ambao husimamishwa na polisi na kuhojiwa, kukaguliwa kimwili na kudhalilishwa ni maradufu ikilinganishwa na ya raia weupe wanaokabiliwa na vitendo kama hivyo.

Megan na Harry wakiwa katika mahojiano yaliyofichua ubaguzi mkubwa unaofanyika katika Kasri la Buckingham

Samuel Etienne ambaye ni mwandishi anasema kuhusu suala hilo kwamba: Ubaguzi wa rangi ni jambo la kawaida kabisa na la kimfumo nchini Uingereza na hilo linaonekana wazi katika matamshi na vitendo vya viongozi wa nchi hiyo dhidi ya 'watu wengine.' Ubaguzi wa rangi pia unaoonekana wazi katika mifumo ya masomo, kazi na afya  na hivi sasa kuhusu mapambano dhidi ya janga la corona.

Matamshi ya Megan Markle na ufichuaji wake kuhusu ubaguzi wa rangi katika kasri la ufalme wa Uingereza kwa mara nyingine umeweka wazi muendelezo wa imani na itikadi za ubaguzi wa rangi zinazotekelezwa katika ufalme huo. Amesema kuwa wengi wa wakazi wa Kasri la Buckingham si tu kuwa walikuwa na wasiwasi kuhusu rangi ya mtoto wake Archie bali hata walitaka kumnyima haki ya urithi wa kifalme na vilevile kutomdhaminia usalama wake. Hata kama hivi sasa vyombo vya habari vya Uingereza vinafanya juhudi kubwa kwa ajili ya kufunika ukweli huo unaotawala katika jamii ya Uingereza lakini inaonekana kuwa ushahidi uliopo unathibitisha wazi madai ya Megan ya kukita mizizi ubaguzi wa rangi katika mfumo wa ufalme wa nchi hiyo.

 

Tags