Jul 26, 2021 02:37 UTC
  • Bunge la Ufaransa lapitisha muswada wa chuki dhidi ya Uislamu

Bunge la Ufaransa Ijumaa lilipitisha muswada wenye chuki na ulio dhidi ya Uislamu uliopewa jina la eti 'mapambano dhidi ya wanaotaka kujitenga' licha ya kuwepo upinzani wa vyama kadhaa vya mrengo wa kushoto dhidi ya muswada huo.

Serikali ya Ufaransa imedai kuwa muswada huo ni muhimu kwa ajili ya kulinda misingi ya usekulari katika nchi hiyo ya Magharibi lakini wapinzani wanasema muswada huo unapinga wazi misingi ya uhuru wa kuabudu. Baada ya kujadiliwa kwa muda wa miezi saba katika seneti na bunge la kitaifa la Ufaransa hatimaye muswada huo umepitishwa kwa kura 49 za 'ndio', 19 za 'hapana' na 5 ambazo hazikuegemea upande wowote.

Akizungumzia suala hilo, Jean-Luc Mélenchon kiongozi wa moja ya vyama vya mrengo wa kushoto vya Ufaransa amesema kwamba muswada huo unapinga moja kwa moja maoni ya wananchi na vilevile Uislamu. Vyama vikuu vya upinzani ikiwa ni pamoja na Chama cha Kisoshalisti, Chama cha Jamhuri na Chama cha Kikomunisti vyote vimepinga muswada huo.

Kwa mujibu wa muswada huo, tokea sasa serikali ya Paris itakuwa na uwezo mkubwa wa kusimamia na kudhibiti shughuli za misikiti na shule za kidini na pia unapinga Waislamu kuoa wanawake zaidi ya mmoja na pia ndoa za kulazimishwa. Muswada huo pia unaipa serikali uwezo wa kusimamisha kwa muda au kupiga marufuku kabisa shughuli zinazoendeshwa katika vituo vya Kiislamu na kiutamaduni na mafundisho maalumu yanayotolewa katika vituo hivyo.

Rais Macron wa Ufaransa, mwenye chuki kubwa dhidi ya Uislamu

Kuanzia sasa mfumo wa usekulari wa Ufaransa ambao unawataka watumishi wote wa serikali kutodhihirisha kazini mielekeo yoyote ya kisiasa, kifalsafa na kidini, sasa utatekelezwa kwa nguvu zaidi. Hii ni katika hali ambayo Waislamu wengi wa Ufaransa wanaamini kwamba muswada huo unabana uhuru wao wa kuabudu na kwamba unawalenga kwa njia tofauti. Ni wazi kuwa Ufaransa ina sheria za kutosha za kupambana na kile kinachotajwa kuwa utumiaji mabavu na ugaidi.

Wapainzani wanasema muswada huo umechochewa na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwa ajili ya kupata uungaji mkono wa wahafidhina na wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia wa nchi hiyo katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Katika uwanja huo Abdullah Al-Shayeji, mhadhiri wa chuo kikuu nchini Kuwait anasema: Kuongezeka uadui wa usekulari dhidi ya Uislamu huko Ufaransa kumechochea misimamo mikali na ya kupindukia mipaka kati ya Rais Macron na Marin Le Pen kiongozi wa wafuasi wenye misimamo mikali wa mrengo wa kulia, na hatimaye kumfanya Macron achukue hatua hiyo kwa ajili ya malengo ya uchaguzi.

Mwenendo wa chuki na mashinikizo dhidi ya Uislamu na Waislamu wa serikali ya Ufaransa umekuwa ukiongezeka katika miaka ya karibuni. Siasa za Macron zimesimama katika msingi wa 'usekulari wa hujuma' ambao unahujumu moja kwa moja misingi na nembo za kidini katika jamii. Wakosoaji wa muswada huo wa eti 'mapambano dhidi ya wanaotaka kujitenga' na ambao karibuni umepasishwa katika bunge la nchi hiyo wanaamini kuwa, Macron na serikali yake wameshinikiza na kupasisha muswada huo bungeni kwa ajili ya malengo ya kisiasa na kuongeza chuki na mashinikizo dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.

Kimsingi Macron hana msimamo wowote chanya kuhusiana na Uislamu bali amekuwa akitumia kila fursa inayopatikana kwa ajili ya kudhihirisha uadui wake dhidi ya Uislamu na Mtume Mtukufu (saw). Suala hilo lilidhihirika wazi kufuatia uungaji mkono wake kwa vikatuni vya kumdhalilisha Mtume (saw) vilivyochapishwa na jarida moja la nchi hiyo, kufukuzwa Waislamu Ufaransa, kufungwa misikiti na vituo vyao vya kidini na kiutamaduni na sasa kupitishwa muswada wa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, ambapo yote hayo yanalenga kudhoofisha Uislamu katika jamii ya Ufaransa.

Wanawake Waislamu wa Ufaransa waandamana kutetea thamani za dini yao

Masoud Shajareh, Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu anasema: Macron anaushambulia wazi Uislamu na kudai kwamba unakabiliwa na mgogoro katika hali ambayo kwa hakika ni siasa za Ufaransa na wanasiasa wengine walio na msimamo kama wake ndio walio kwenye mgogoro.

Raia wa Ufaransa na hasa Waislamu wamekuwa wakifanya maandamano mengi kulalamikia dhulma wanayofanyiwa na serikali ya Paris na hasa kuhusiana na muswada uliopasishwa karibuni na bunge la nchi hiyo wakisema kuwa muswada huo unabana uhuru wao wa kuabudu na kuwafanya wote kuwa washukiwa wa vitendo vya ugaidi na waonekane kuwa wanaotaka kujitenga na jamii ya Ufaransa.

Tags