Maelfu waandamana Niger wakitaka kufukuzwa askari wa US, Ufaransa
Maelfu ya wananchi wa Niger wamefanya maandamano katika mji mkuu Niamey, wakitaka kufukuzwa nchini humo mara moja wanajeshi wa Marekani na Ufaransa.
Wananchi hao wa Niger wanaounga mkono mapinduzi yaliyofanyika karibuni, huku wakitaka Wamagharibi wasiingilie mambo ya ndani ya nchi yao, walipeperusha bendera ya Urusi na kutoa nara na kaulimbiu dhidi ya Ufaransa na Marekani.
Waandamanaji hao wamesema taifa hilo linapaswa liachwe lijiendeshee mambo yake, na kuzitaka nchi za Magharibi kukoma kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo.
Nchi hiyo ya Afrika Magharibi ina rasilimali nyingi za asili, hususan urani, almasi, dhahabu na makaa ya mawe; migodi ambayo siku zote imekuwa muhimu kwa nchi za Magharibi.

Wananchi wa Niger walioshiriki maandamano hayo nje ya majengo ya Bunge la nchi hiyo wamesisitiza kuwa, ubeberu na sera za uingiliaji za Marekani, Ufaransa na Umoja wa Ulaya zimesambaratisha kikamilifu uhuru wa nchi hiyo ya Kiafrika.
Maandamano hayo yanajiri siku chache baada ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, kutangaza kuwa wanajeshi 1,000 wa nchi hiyo wametumwa tena nchini Niger; baada ya kupinduliwa na kukamatwa Rais wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, Mohamed Bazuom.