Feb 09, 2024 08:10 UTC
  • Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan
    Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan

Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Sudan jana Alhamisi ilikanusha taarifa iliyotolewa na Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Martin Griffiths, ambaye alidokeza kuwa Rais wa Baraza Kuu la Utawala nchini Sudan, Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan, amekubali kukutana na Kamanda wa Kikosi cha Msaada wa Haraka, Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti), nchini Uswisi, kwa madhumuni ya kuwezesha kuwasili kwa misaada kwa watu walioathirika na vita huko Sudan.

Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Sudan imeliambia gazeti la Al-Ahdath kwamba Al-Burhan hajapokea simu kutoka kwa Griffiths kuhusiana na suala hilo, akisisitiza kwamba mambo yote yanayohusiana na misaada yanasimamiwa na Luteni Jenerali Ibrahim Jaber.

Umoja wa Mataifa ulitangaza siku ya Jumatano kwamba pande mbili katika vita vya Sudan zimekubaliana kufanya mkutano, ambao huenda ukafanyika nchini Uswisi, kujadili suala la kuwasilisha misaada ya kibinadamu kwa waathiriwa wa vita.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu Martin Griffiths alisema kuwa amewasiliana na Al-Burhan na Hemedti kuhusu suala la kufanya mkutano baina ya wawakilishi wa pande mbili zinazozozana nchini Sudan kujadili kadhia ya misaada ya kibinadamu.

Griffiths alithibitisha - katika taarifa alizotoa kwenye mkutano na waandishi wa habari - kwamba pande zote mbili zilikubaliana na suala hilo.

Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanaendelea nchini Sudan tangu Aprili 15, kati ya vikosi vya jeshi vinavyoongozwa na Al-Burhan na Vikosi vya Msaada wa Haraka chini ya uongozi wa Mohamed Hamdan Dagalo. Hadi sasa mapigano hayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu. Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa inasema takriban watu 10,000 kati yao wameuawa huko Darfur, magharibi mwa Sudan.

Wakimbizi wa ndani Sudan

Taarifa zinasema kuwa Wasudani milioni 25 wanateseka kwa njaa kutokana na vita hivyo vya kuwania madaraka baina ya majenerali hao wa kijeshi.

Tags