Watu 5 wapoteza maisha katika maandamano ya ghasia nchini Msumbiji
Polisi ya Msumbiji imeripoti kuwa watu wasiopungua watano wamepoteza maisha na wengine watatu wamejeruhiwa vibaya katika maandamano ya ghasia katika miji ya Maputo, Nampula na Zambezia.
Orlando Mudumane Msemaji wa Kamandi Kuu ya Polisi ya Msumbiji ameeleza kuwa ghasia ziliibuka kati ya polisi na waandamanaji waliokuwa wamejizatiti kwa mawe, visu na mapanga.
Amesema kuwa waandamaji hao walikusanyika kufuatia wito wa Venancio Mondlane, mgombea urais aliyeshindwa katika uchaguzi wa karibuni, ambaye amedai kuwa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 9 mwaka huu yalijaa udanganyifu na hivyo kujitangaza mshindi.

Akiwa nchini Afrika Kusini ambako amepewa hifadhi, Mondlane amewataka wananchi wa Msumbiji kufanya maandamano ya nchi nzima kwa muda wa wiki moja kuanzia Disemba 4 hadi 11 ili kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais.
Pilipe Nyusi, Rais anayemaliza muda wake wa Msumbiji, ameonya kuwa mandamano hayo ya ghasia na vurugu yanaweza kuvuruga malipo ya mishahara ya sekta ya umma, hasa kwa walimu na wauguzi kutokana na Msumbiji kutokuwa na msaada wa fedha kutoka nje.
Watu walioshuhudia wameeleza kuwa katika eneo la Matola, maandamano yalipamba moto na kuibua ghasia baada ya afisa polisi kumjeruhi vibaya kwa risasi mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 13. Polisi huyo hakuwa amevalia sare za polisi.