Ripoti: Uganda yaongoza kwa visa vya uhalifu Afrika Mashariki
Utafiti mpya umefichua kuwa, Uganda ndiyo inayoongoza kwa visa vya uhalifu wa kutumia silaha za moto katika kanda ya Afrika Mashariki.
Ripoti ya Kituo cha Kieneo cha Kudhibiti Matumizi ya Silaha Ndogo (RECSA) imebanisha kuwa, kati ya mwaka 2010 hadi Machi mwaka huu, Uganda imerekodi kesi 34, 512 za uhalifu wa kutumia silaha kama bunduki na bastola. Katika kipindi hicho, Burundi ilirekodi visa 26, 041 huku Kenya ikirekodi kesi 12,877.
Tanzania ilirekodi kesi 9, 646 za matumizi ya silaha za moto kinyume cha sheria, huku Rwanda ikitajwa kuwa nchi iliyorekodi visa vichache vya uhalifu kwa kutumia silaha hizo katika muda huo, kwa kunakili kesi 421.
Theoneste Mutsindashyaka, Katibu Mkuu wa Kituo cha Kieneo cha Kudhibiti Matumizi ya Silaha Ndogo (RECSA) ameipongeza Rwanda kwa kurekodi visa vichache vya uhalifu kwa kutumia silaha za moto sambamba na kuzuia uenezaji wa silaha nyepesi nchini humo.
Amesema magendo na usambamazaji wa silaha hizo umechangia pakubwa kuchochea machafuko katika baadhi ya nchi za Afrika mbali na kuyumbisha usalama, amani na maendeleo ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katibu Mkuu wa RECSA ameongeza kuwa, silaha hizo zilitumika kinyume cha sheria katika uhalifu mbalimbali kama vile hujuma za kigaidi, ujangili, wizi wa mabavu na wizi wa mifugo.