Kampuni ya Uingereza yalazimika kuondoka Tunisia baada ya kukabiliwa na maandamano
Kampuni moja ya mafuta na gesi ya Uingereza iliyokuwa ikiendesha ghughuli zake nchini Tunisia imelazimika kuondoka nchini humo kufuatia malalamiko ya wananchi.
Kampuni hiyo ya Petrofac ambayo inasimamia visima kadhaa vya gesi huko Tunisia imelazimika kuondoka nchini humo kufuatia kuongezeka maandamano na malalamiko ya wananchi dhidi yake kwa miezi kadhaa sasa. Imeelezwa kuwa kampuni hiyo ilikuwa ikidhamini karibu asilimia13 ya mahitaji ya gesi ya Tunisia, na wakati huo huo ilikuwa ikidhamini nishati ya gesi na mafuta kwa mikoa miwili nchini humo. Kusimama kwa shughuli za kampuni ya Petrofac ya Uingereza huko Tunisia, kumeipelekea serikali ya Tunisia kuagiza gesi kutoka Algeria.
Maandamno ya vijana wa Kitunisia tangu mwezi Januari mwaka huu yamevuruga uzalishaji wa gesi katika kisima cha Chergui katika Kisiwa cha Kerkennah kusini mwa Tunisia ambako Petrofac inamiliki hisa ya asilimai 45, na iliyosalia inamilikiwa na Kampuni ya Taifa ya Tunisia.
Kampuni hiyo kwa siku ilikuwa ikipata hasara ya dola elfu sitini kutokana na kuendelea ukosefu wa amani na matatizo ya kiuchumi huko Tunisia.