Kushambuliwa Waislamu na jeshi la Nigeria
Katika kuendelea vitendo vya mauaji vya jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu, kwa mara nyingine Waislamu wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika wameshambuliwa na jeshi.
Idadi ya mashahidi waliouawa katika shambulio la jeshi dhidi ya Waislamu wa Kishia katika mji wa Kano imeongezeka na kufikia mia moja. Jana Jumatatu, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ilitangaza kuwa, makumi ya Waislamu walishambuliwa na kuuawa na jeshi la Nigeria wakati walipokuwa katika shughuli ya kidini nje kidogo ya mji wa Kano ulioko kaskazini mwa Nigeria. Mchafuko yalianza pale, polisi ya Nigeria ilipoamua kutumia nguvu kuwatawanya Waislamu waliokuwa wakitembea kutoka Kano kwenda Kaduna katika siku hizi za kukaribia kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein as.
Shambulio hilo limefanyika katika hali ambayo, Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu imeitaka serikali ya Nigeria idhamini usalama wa Waislamu katika kipindi chote cha kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein as. Mwezi uliopita wanajeshi wa Nigeria walishambulia marasimu ya Ashura katika mji wa Funtua katika jimbo la Katsina ambapo kwa uchache Waislamu 20 wa Kishia waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Vitendo vya mauaji na utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu nchini Nigeria ni kwa muda sasa vimeshika kasi nchini humo ambapo Waislamu wamekuwa wakishambuliwa mara kwa mara wakiwa katika shughuli zao za kidini. Mashinikizo na mauaji ya jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu yalianza Disemba mwaka jana baada ya kushambulia Husseiniyyah ya Baqiyatulllah na makazi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky mjini Zaria.
Tangu wakati huo, kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria angali anashikiliwa na vyombo vya usalama huku hali yake ya kiafya ikiripotiwa kuwa mbaya. Licha ya juhudi na miito ya kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, lakini kiongozi huyo angali anashikiliwa korokoroni na harakati zote za kutaka mwanazuoni huyo aachiliwe huru hadi sasa bado hazijazaa matunda. Femi Falana, wakili wa Sheikh Ibrahim Zakzaky amenukuliwa mara kadhaa akisema kuwa, hali ya kiafya ya kiongozi huyo wa Kiislamu si ya kuridhisha na kwamba, serikali na vyombo vya usalama vya nchi hiyo haviko tayari kutoa maelezo kuhusiana na jambo hilo.

Jeshi la Nigeria limeongeza mashinikizo dhidi ya Waislamu katika hali ambayo, nchi hiyo kwa sasa inakabiliwa na matatizo chungu nzima. Harakati za kundi la kigaidi la Boko Haram katika maeneo mbalimbali ya nchio hiyo, ukame na uhaba wa chakula kwa raia wa maeneo ya kaskazini mwa Nigeria, kuyakimbia makazi yao raia kutokana na mashambulio ya kigaidi, kutoridhika na utendaji wa serikali kuu jimbo la kusini mwa nchi na milipuko ya mara kwa mara katika taasisi za mafuta inayotekelezwa na makundi ya waasi ni miongoni mwa matatizo yanayoikabili Nigeria kwa sasa.
Uingiliaji wa baadhi ya madola ya kigeni katika eneo la magharibi mwa Afrika umezusha hitilafu na mifarakano. Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi hizo, ambapo kutokana na siasa zake kugonga mwamba katika Mashariki ya Kati, hivi sasa imepanua harakati zake barani Afrika na imo katika kuzusha hitilafu na mifarakano.
Utawala wa Kizayuni nao baada ya kuzidi kutengwa katika Mashariki ya Kati na kuzidi kufahamika siasa zake za kupenda vita, sasa umekuja na utendaji mpya wa kutaka kuwa na ushawishi barani Afrika. Mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Nigeria nayo yanapaswa kutathminiwa katika uwanja huu.

Katika mazingira kama haya, endapo serikali ya Nigeria itaendeleza hatua zake za kutumia mabavu dhidi ya Waislamu kupitia jeshi lake, sio tu kwamba, matatizo ya nchi hiyo hayatapatiwa ufumbuzi, bali kutashuhudiwa pengo kubwa baina ya serikali na jamii ya Waislamu nchini humo. Hii ni katika hali ambayo, Nigeria inahitajia mno umoja kwa ajili ya kuendesha vita vya kila upande dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram na kurejesha amani na uthabiti katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.