Magaidi wa Kikristo waua askari wa kulinda amani wa UN, CAR
(last modified Wed, 26 Jul 2017 07:52:38 GMT )
Jul 26, 2017 07:52 UTC
  • Magaidi wa Kikristo waua askari wa kulinda amani wa UN, CAR

Kundi la kigaidi la Kikristo la Anti-Balaka limeua askari wawili wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA.

Taarifa iliyotolewa na MINUSCA imesema wanajeshi hao raia wa Morocco wameuawa baada ya kutekwa nyara na wanachama wa genge hilo la kigaidi, katika mji wa Bangassou, yapata kilomita 700 mashariki mwa mji mkuu Bangui.

Imeongeza kuwa, askari hao wa kulinda amani wa UN walikuwa wanateka maji kwa ajili ya kuwapelekea raia wanaoishi viungani mwa mji huo, wakati walipovamiwa na magaidi hao wa Kikristo.

Wanajeshi wa MINUSCA, CAR

Taarifa ya Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati imeongeza kuwa, hili ni shambulizi la pili dhidi ya wanajeshi wa kikosi hicho wiki hii.

Mwezi Mei mwaka huu, watu 115 aghalabu yao wakiwa wafuasi wa dini ya Kiislamu waliuawa na wapiganaji wa Anti-Balaka, katika mji wa Bangassou, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. 

Mashirika kadhaa ya kigeni ya kutoa misaada ya kibinadamu yamesimamisha shughuli zao katika mji huo, kutokana na kushtadi machafuko.