WHO yatahadharisha kuhusu ugonjwa wa virusi vya Marburg Kenya na Uganda
Shirika la Afya Duniani (WHO) limewatahadharisha wageni wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Mt Elgon juu ya hatari ya kupatwa na ugonjwa wa virusi vya Marburg.
Taarifa WHO inasema hifadhi hiyo ambayo iko katika mpaka wa Kenya na Uganda, ina mapango ya popo-matunda ambao hujulikana kuhamisha na kuambukiza virusi vya Marburg.
Mapango hayo na ukaribu wake kwa eneo lililoathiriwa nchini Uganda, yanazidisha hatari ya virusi vya Marburg kuvuka mpaka na kuenea kati ya wanadamu na mapopo katika nchi hizo mbili.
Taarifa ya WHO imesema watalii wanaotembelea Mlima Elgon, ikiwa ni pamoja na mapango na maeneo ya jirani, wanapaswa kuonywa na kupewa ushauri sahihi wa kuwa na tahadhari.
Tahadhari hiyo imetolewa wakati Shirika la Afya Dunia (WHO), mashirika mengine ya kimataifa, na serikali za Kenya na Uganda, zimetayarisha timu za kudhibiti kasi ya kuenea kwa virusi vya Marburg katika nchi za Uganda na Kenya.
Waziri wa Afya wa Uganda Dakta Jane Ruth Aceng amethibitilisha kufariki dunia watu wawili kutokana na virusi vya Marburg nchini humo. Idara ya utafiti wa virusi vya Marburg nchini Uganda imesema kuwa, ugonjwa huo unaua haraka kama Ebola.
Virusi vya Marburg vinaweza kumuuwa mtu mwenye afya katika kipindi cha wiki moja tu baada ya kuanza kutapika na kuharisha na hatimaye kutokwa damu ndani kwa ndani. Ugonja huo hauna tiba.
Uganda imeshawahi kukumbwa na milipuko ya homa za Ebola na Marburg katika siku za nyuma, japokuwa milipuko hiyo ilidhibitiwa haraka.