Maandamano ya kuwapinga Wazayuni yaendelea nchini Tunisia
Wananchi wa Tunisia kwa mara nyingine wameshiriki katika maandamano makubwa ya kupinga jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Gazeti la al Quds al Arabi linalochapishwa mjini London Uingereza limeripoti habari hiyo na kusema kuwa mamia ya wananchi wa Tunisia wamefanya maandamano mbele ya bunge la nchi hiyo wakilitaka lipasishwe sheria ya kulihesabu suala la kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni uhalifu.
Waandamanji wametoa nara za kuunga mkono Palestina na kutangaza upinzani wao kwa uamuzi wa hivi karibuni wa rais wa Marekani Donald Trump aliyeitambua rasmi Quds kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni.
Waandamanaji hao aidha wamepiga nara inayosema: "Kulihesabu kuwa ni uhalifu suala la kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel ni jukumu la kila mtu." Vile vile wamesema: "Quds ni mji mkuu wa milele wa Palestina" na "Palestina itakombolewa."
Jumuiya ya waungaji mkono wa Palestina nchini Tunisia, siku ya Jumatano iliwasilisha muswada katika bunge la nchi hiyo unaolitaka likihesabu kuwa ni uhalifu kitendo chochote cha kujaribu kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel.
Itakumbukwa kuwa tangu tarehe 6 mwezi huu wa Disemba, wakati rais wa Marekani, Donald Trump alipochukua hatua hiyo ya kiuadui ya kuitangaza Baytul Muqaddas kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, maandamano yameenea katika kila kona ya dunia yakimlaani Trump kwa uadui wake huo na kuiunga mkono Quds yenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu.