Trump aelekeza vita vya kibiashara Afrika, Rwanda yajibu mapigo
Baada ya kuanzisha vita vya kibiashara dhidi ya nchi za Asia na Ulaya na kupata jibu kali, sasa Rais wa Marekani Donald Trump anaonekena kueelekeza vita hivyo kwa nchi za Afrika.
Trump ametangaza kusimamisha kwa muda usiojulikana mpango wa kutozitoza ushuru nguo zinazoingia nchini humo kutoka Rwanda, uliokuwa ukitekelezwa chini ya sheria ya African Growth and Opportunity.
Trump ametangaza kuchukua hatua hiyo kama radiamali kwa hatua ya Rwanda ya kuongeza ushuru wa forodha uliokuwa ukitozwa nguo kuu kuu (mitumba) zinazoingizwa nchini humo kutoka Marekani.
Rwanda ambayo inajaribu kuponya makovu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, imesema imeongeza ushuru wa forodha nguo hizo kuu kuu kutoka Marekani kwa lengo la kuimarisha soko la kuzalisha nguo nchini humo.
Trump amechukua hatua hiyo wiki chache baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Paul Kagame katika Mkutano wa Uchumi Dunia na kumtaja Mwenyekiti huyo mpya wa Umoja wa Afrika kama 'rafiki'.
Duru za habari zimedokeza kuwa, yumkini nchi nyingine za Afrika zitalengwa hivi karibuni katika vita hivyo vya kibiashara vya Marekani, hususan Tanzania na Uganda ambazo zimetangaza azma ya kupiga marufuku nguo za mitumba kufikia mwaka 2019.
Amri ya Trump ya Machi 22 mwaka huu ya kuzipandishia ushuru mpya wa forodha bidhaa za chuma na alumini za China iliyotolewa kwa lengo la kudhoofisha ongezeko la kiuchumi la Beijing, ndio ilizusha vita vya biashara na nchi wazalishaji wakubwa yakiwemo pia mataifa ya Ulaya.