UN yamuwekea vikwazo Waziri wa Ulinzi wa Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45044-un_yamuwekea_vikwazo_waziri_wa_ulinzi_wa_sudan_kusini
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetangaza kumuwekea vikwazo Waziri wa Ulinzi wa Sudan Kusini, Kuol Manyang Juk kutokana na kile lilichodai kuwa ni kitendo cha afisa huyo wa Juba kukiuka makubaliano ya usitishaji vita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 27, 2018 09:17 UTC
  • UN yamuwekea vikwazo Waziri wa Ulinzi wa Sudan Kusini

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetangaza kumuwekea vikwazo Waziri wa Ulinzi wa Sudan Kusini, Kuol Manyang Juk kutokana na kile lilichodai kuwa ni kitendo cha afisa huyo wa Juba kukiuka makubaliano ya usitishaji vita.

Baada ya kufanya kikao cha kujadili mgogoro wa Sudan Kusini mjini New York hapo jana, baraza hilo limesema katika taarifa kwamba, chini ya amri ya Jenerali Juk, vikosi vya SPLA vimekiuka makubaliano ya usitishaji vita na uhasama ya mwaka 2017, na vimekuwa vikichochea mapigano na kuhatarisha maisha ya raia wasio na hatia.

Taarifa hiyo ya UNSC imeongeza kuwa, Waziri wa Ulinzi wa Sudan Kusini alilipa msaada wa kijeshi kundi la wapiganaji wa SPLM ili kushambulia Pagak, makao makuu ya waasi katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD hivi karibuni ilitangaza kuwa inaunga mkono hatua ya kuwekewa vikwazo viongozi na shakhsia wote wanaokwamisha jitihada za kupatiwa ufumbuzi mgogoro nchini Sudan Kusini.

Wapiganaji watiifu kwa serikali ya Sudan Kusini

Mjumbe Maalumu wa IGAD nchini Sudan Kusini, Ismail Wais amesema asasi hiyo ya kikanda inaunga mkono hatua zote za kufunga akaunti za benki za wanasiasa na makamanda wa zamani wa kijeshi wanaochochea mapigano katika nchi hiyo changa zaidi duniani.

Sudan Kusini ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2013, baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake. Vita hivyo vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.