Somalia yaitaka UN iiondolee vikwazo vya silaha
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Somalia ameutaka Umoja wa Mataifa kuondoa vikwazo vya muda mrefu vya silaha dhidi ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Ahmed Awadh Issa ametoa mwito huo akihutubia mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na kuongeza kuwa, serikali changa ya Mogadishu imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab.
Amebainisha kuwa, japokuwa safari ya kurejesha amani na utulivu nchini Somalia bado ni ndefu, lakini idiolojia ya genge la kigaidi la al-Shabaab inaendelea kufifia siku baada ya nyingine na kwamba vijana hawajiungi tena na kundi hilo.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Somalia ameongeza kuwa, baadhi ya makanda wa ngazi za juu wa kundi la al-Shabaab wamekumbatia msamaha wa serikali na kuamua kuweka silaha chini na kujisalimisha kwa vyombo vya usalama.
Wiki mbili zilizopita, Michael Keating, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia alisema kuwa, hali ya Somalia kiujumla imeboreka ikilinganishwa na miezi kadhaa iliyopita licha ya kuwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ingali inakabiliwa na changamoto nyingi.
Somalia ilitumbukia katika mapigano na machafuko ya ndani tangu ilipoondolewa madarakani serikali ya Mohamed Siad Barre mwanzoni mwa muongo wa 1990. Mbali na harakati za kundi la kigaidi la al-Shabab kuwa tatizo kuu nchini Somalia, nchi hiyo inakabiliwa pia na ukame na baa la njaa.