Ndege za kivita za kigeni zimehusika katika mashambulio ya Tripoli
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya amesema kuwa ndege za kigeni zilishiriki katika mashambulio ya hivi karibuni katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli.
Waziri Fathi Bashagha amesema kuwa serikali ya nchi hiyo ina ushahidi na nyaraka za kuthibitisha ushiriki huo wa ndege za kigeni katika mashambulio ya Tripoli na kuongeza kuwa umakini uliotumika katika mashambulio hayo unathibitisha wazi kwamba ndege hizo ni za nchi mbili za Kiarabu. Fathi Bashagha ameendelea kusema kuwa mashambulio yaliyofanywa na askari watiifu kwa Khalifa Haftar, kamanda wa askari wanaojiita kuwa wa Jeshi la Kitaifa la Libya mjini Tripoli yamepelekea kuhuishwa kwa makundi ya kigaidi nchini humo. Waziri huyo wa Mambo ya Ndani wa Libya huku akiashiria kimya kikubwa cha jamii ya kimataifa kuhusiana na mashambulio hayo ya adui katika mji mkuu huo ameitaka Ufarasnsa kuheshimu thamani inazodai kuwa inaziheshimu na kukoma kushirikiana na kamanda muasi Khalifa Haftar katika mashambulio yake dhidi ya mji wa Tripoli.
Baadhi ya nchi kubwa za Magharibi na za Kiarabu pamoja na Umoja wa Mataifa zimeunga mkono kwa njia isiyo ya moja kwa moja mashambulio hayo ya kijeshi yanayofanywa na askari wa Haftar katika mji mkuu wa Libya Tripoli, ulio magharibi mwa nchi hiyo ya Kiafrika. Haftar amekuwa akiungwa mkono kieneo na nchi tatu za Kiarabu za Misri, Saudi Arabia na Imarati zinazotajwa kuwa 'pembetatu ya shari' katika eneo.
Jeshi la Haftar ambalo lina makao makuu yake mashariki mwa Libya lilianzisha mashambulizi makali dhidi ya ngome za serikali inayotambulika kimataifa ya Umoja wa Kitaifa mjini Tripoli mnamo tarehe nne mwezi huu wa Aprili. Mashambulio hayo kufikia sasa yamepelekea watu 270 kupoteza maisha, 1300 kujeruhiwa na wengine elfu 35 kuwa wakimbizi.