Makumi wahofiwa kufa maji baada ya boti yao kuzama pwani ya Tunisia
Makumi ya wahajiri wanahofiwa kupoteza maisha katika ajali ya boti iliyotokea katika pwani ya Tunisia.
Mongi Slim, afisa wa Shirika la Hilali Nyekundu la Tunisia ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, boti hiyo ilizama juzi Jumatano katika pwani ya Zarzis, kusini mashariki mwa Tunisia.
Manusura wanne wameiambia Gadi ya Pwani ya Tunisia kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba watu zaidi ya 70. Naye Vincent Cochetel, Mjumbe Maalumu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR katika eneo la Mediterania amesema boti hiyo ilikuwa imebeba wahajiri zaidi ya 80, na kwamba wanne tu ndo wameweza kunusurika.
Itakumbukwa kuwa mwezi Juni mwaka jana pia, wahajiri 80 walikufa maji baada ya boti yao kuzama katika fukwe za Tunisia, mwezi mmoja baada ya wahajiri wengine 65 kufa maji katika pwani hiyo hiyo ya Tunisia.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri, njia ya majini ya kutoka Libya kuelekea nchi za Ulaya ikiwemo Italia na Malta, ndiyo njia hatari zaidi kwa maafa ya roho za watu inayotumiwa na wahajiri haramu hasa kutoka nchi za Kiafrika kwa safari za kuelekea barani Ulaya kwa lengo la kutafuta maisha mazuri.
Wadadisi wa mambo wanasema mgogoro mkubwa wa wahajiri na wakimbizi unaoshuhudiwa hivi sasa ni matokeo ya siasa za uingiliaji kati za madola ya Magharibi katika nchi za eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika; mgogoro ambao umelihusisha pia bara Ulaya.