Hilali Nyekundu: Walioaga dunia katika ajali ya boti Tunisia wamepindukia 70
Shirika la Hilali Nyekundu la Tunisia limeripoti kuwa, idadi ya watu walioaga dunia katika ajali ya boti iliyotokea katika pwani ya nchi hiyo siku chache zilizopita imeongezeka na kufikia watu 72.
Shirika hilo limetangaza leo Ijumaa kuwa, boti hiyo iliyotokea Libya ikielekea Ulaya ilikuwa imebeba wahajiri zaidi ya 80, kinyume na ilivyodhaniwa hapo awali. Manusura wanne waliiambia Gadi ya Pwani ya Tunisia kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba wahajiri 70.
Mongi Slim, afisa wa Shirika la Hilali Nyekundu la Tunisia ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, boti hiyo ilizama Jumatano ya wiki iliyopita katika pwani ya Zarzis, kusini mashariki mwa Tunisia.
Kadhalika Vincent Cochetel, Mjumbe Maalumu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) katika eneo la Mediterania amethibitisha kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba wahajiri zaidi ya 80 na yumkini wote wamekufa maji ghairi ya manusura wanne.
Itakumbukwa kuwa mwezi Juni mwaka jana pia, wahajiri 80 walikufa maji baada ya boti yao kuzama katika fukwe za Tunisia, mwezi mmoja baada ya wahajiri wengine 65 kufa maji katika pwani hiyo hiyo ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Wadadisi wa mambo wanasema mgogoro mkubwa wa wahajiri na wakimbizi unaoshuhudiwa hivi sasa ni matokeo ya siasa za uingiliaji kati za madola ya Magharibi katika nchi za eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika.