Viwiliwili vya wahajiri 79 waliozama baharini Tunisia vyapatikana
Siku kumi zilizopita, mtumbwi mmoja uliokuwa umejaza wahajirii ulizama karibu na fukwe za Tunisia. Hadi hivi sasa miili 79 ya wahajirii hao imeshaopolewa kutoka baharini.
Mtumbwi huo ulikuwa umebeba watu 86 na ulizama karibu na fukwe za Tunisia tarehe 3 mwezi huu wa Julai katika Bahari ya Mediterranean. Kati ya watu hao 86, ni wanne tu ndio walioweza kuokolowa na askari wa kutoa misaada wa Tunisia, waliobakia wengine wote yaani wahajiri 82 walitoweka.
Mounji Salim, Mkuu wa Hilal Nyekundu ya Tunisia katika mkoa wa Medinine wa kusini mwa nchi hiyo amethibitisha jambo hilo na kusema kuwa, hadi hivi sasa miili 79 ya watu waliozama kwenye ajali hiyo wameshaopolewa kutoka majini na watatu waliobakia hawajapatikana hadi hivi sasa.
Watu wengi hupotea na kuzama bahari kila mwaka katika fukwe za Tunisia wakijaribu kuvuuka kimagendo kuelekea barani Ulaya kwa tamaa ya kupata maisha mazuri.
Wengi wa wahajirii hao ni kutoka nchi za Afrika ambao hujitumbukiza kwenye safari hizo za kifo imma kwa tamaa ya kupata utajiri wa haraka au kukimbia umaskini wa kuchupa mipaka, au machafuko ya kisiasa na kijamii katika nchi zao. Sababu nyingine ni uingiliaji wa madola ya Magharibi katika masuala ya ndani ya nchi za Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini ndiko kunakochochea wimbi hilo la wahajiri haramu.
Itakumbukwa kuwa mwezi Juni mwaka jana pia, wahajiri 80 walikufa maji baada ya mtumbwi wao kuzama katika fukwe za Tunisia, mwezi mmoja baada ya wahajiri wengine 65 kufa maji katika pwani hiyo hiyo ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.