Bunge la Waarabu laitaka Marekani iiondoe Sudan katika orodha ya ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57488-bunge_la_waarabu_laitaka_marekani_iiondoe_sudan_katika_orodha_ya_ugaidi
Bunge la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu limeitaka Marekani iiondoe Sudan kwenye orodha ya Washington ya eti nchi zinazounga mkono ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 25, 2019 08:46 UTC
  • Bunge la Waarabu laitaka Marekani iiondoe Sudan katika orodha ya ugaidi

Bunge la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu limeitaka Marekani iiondoe Sudan kwenye orodha ya Washington ya eti nchi zinazounga mkono ugaidi.

Mwito huo umetolewa na Spika wa Bunge hilo, Mishaal bin Fahm Al-Salami, kwenye barua alizowaandikia Mike Pence, Makamu wa Rais wa Marekani na pia Rais wa Bunge la Seneti, Nancy Pelosi, Spika wa Bunge la Wawakilishi na Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani.

Katika barua hiyo, al-Salami amewaambia maafisa hao wa serikali ya Washington kuhusu azimio lililopasishwa kwa kishindo na Bunge la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mnamo Oktoba 31, la kuitaka Marekani iiondoe Sudan kwenye orodha hiyo mara moja.  

Hii ni katika hali ambayo, Mkuu wa Baraza la Utawala nchini Sudan amesema kuwa, kutoondolewa jina la nchi hiyo katika orodha ya ugaidi, kumewakatisha tamaa raia wa nchi hiyo.

Donald Trump na viongozi wa nchi za Kiarabu

Abdel Fattah al-Burhan ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya Al Jazeera ambapo amesema kuwa, awali serikali ya Khartoum ilikuwa imefanya mazungumzo na Marekani kuhusu suala la kuondolewa Sudan katika orodha ya ugaidi. Hata hivyo upande wa Marekani unadai kuwa ina sheria na hatua maalumu za kutekeleza suala hilo. Itakumbukwa kuwa Oktoba 2017 serikali ya Marekani katika muamala na serikali ya Rais Omar al-Bashir iliifutia vikwazo vya kiuchumi na kibiashara iliyoiwekea nchi hiyo kuanzia mwaka 1997.

Washington imegoma kufuta jina la Sudan katika orodha ya nchi zinazodaiwa na Marekani kuunga mkono ugaidi kutokana na nchi hiyo kumpokea Osama bin Laden, kinara wa kundi la Al-Qaidah hapo mwaka 1993.