Rais: Zimbabwe haitarejea katika matumizi ya sarafu ya dola ya Marekani
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amesema licha ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kukabiliwa na mtikisiko mkubwa wa kiuchumi, lakini haitarejea katika matumizi ya sarafu ya dola ya Marekani.
Rais Mnagangwa alisema hayo jana Ijumaa katika mkutano wa kila mwaka wa chama tawala ZANU-PF na kuongeza kuwa, "Hakuna taifa linaloweza kustawi bila kuwa na safaru yake."
Ameeleza bayana kuwa, ingawaje kuna watu wengi wanapinga mpango huo, lakini serikali yake haitaruhusu sarafu za kigeni ikiwemo dola ya Marekani kuvuruga mkondo wa ustawi wa uchumi wa nchi hiyo.
Sarafu ya dola ya Zimbabwe imepoteza asilimia 61 ya thamani yake tangu ilipozinduliwa upya mnamo Juni mwaka huu, hatua ambayo imepelekea mfumko wa bei nchini humo ufikie kiwango cha asilimia 440.
Matatizo ya kifedha yaliikumba nchi hiyo na kuilazimisha ianze kutumia sarafu mbalimbali za kigeni ikiwemo dola ya Marekani tangu mwaka 2009; baada ya kiwango cha mfumko kufikia kilele chake kwa asilimia 500 na kusasabisha dola ya Zimbambwe kutokutumika.
Hii ni katika hali ambayo, licha ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Rais Emmerson Mnangagwa kuiomba Marekani iifutie Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi, lakini Washington inasisitiza kuwa Marekani haitaondoa vikwazo ilivyoiwekea Zimbabwe hadi pale serikali mpya ya Rais Emmerson Mnangagwa itakapodhihirisha kuwa inabadili mielekeo yake.
Marekani inadai kuwa, sera za Rais Mnangagwa zingali 'tishio lisilo la kawaida' kwa sera za nje za Washington.