Umoja wa Mataifa watakiwa uunge mkono usitishaji vita katika maeneo ya mapigano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60819-umoja_wa_mataifa_watakiwa_uunge_mkono_usitishaji_vita_katika_maeneo_ya_mapigano
Nchi za Tunisia na Ufaransa zimelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuunga mkono na kuafiki azimio la kusimamisha vita haraka katika maeneo ya mapigano duniani kama sehemu ya vita dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 06, 2020 20:09 UTC
  • Umoja wa Mataifa watakiwa uunge mkono usitishaji vita katika maeneo ya mapigano

Nchi za Tunisia na Ufaransa zimelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuunga mkono na kuafiki azimio la kusimamisha vita haraka katika maeneo ya mapigano duniani kama sehemu ya vita dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.

Tunisia hivi sasa ni mmoja wa wanachama 10 wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa huku Ufaransa ikiwa ni moja ya nchi tano zenye kura ya veto katika baraza hilo. Nchi hizo mbili zimewasilisha muswada wa azimio hilo zikiwa na matumaini ya kuungwa mkono na wajumbe wengine wote wa baraza hilo na iwapo azimio litatolewa, basi litakuwa la kwanza la Baraza la Usalama baada ya kuzuka ugonjwa wa corona.

Pamoja na hayo wanadiplomasia wanasema kuwa, kwa vile hivi sasa pana ugomvi baina ya Marekani na China kuhusu Shirika la Afya Duniani (WHO), kuna uwezekano mkubwa upigaji kura ukakwama katika hatua yake ya awali kabisa.

Mapigano yamesababisha hasara kubwa nchini Libya

 

Muswada wa azimio hilo lililopendekezwa na Tunisia na Ufaransa unahusu kusimimshwa vita haraka katika maeneo yenye mapigano mengi kama Syria, Yemen, Libya, Sudan Kusini na Kongo na shabaha yake ni kuzitaka pande zote hasimu zisimamishe vita kwa angalau siku 30.

Mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Aprili, rais wa Marekani, Donald Trump, alilikatia misaada Shirika la Afya Duniani WHO kwa madai ya kushindwa kuzuia kuenea kirusi cha corona mara baada ya kugunduliwa kesi ya kwanza huko Wuhan, China.

Hata hivyo China imeliunga mkono kikamilifu shirika hilo na inasisitiza kuwa, mchango wa WHO unapaswa kuingizwa katika kila azimio na hatua ya kimataifa ya kupambana na corona.