Ethiopia yakiri kutungua ndege ya Kenya katika ardhi ya Somalia
Askari wa jeshi la Ethiopia wamekiri kuwa walitungua kimakosa ndege ndogo ya Kenya iliyokuwa imebeba misaada na vifaa vya kupambana na janga la corona katika mji wa Bardale, kusini mwa eneo la Bay nchini Somalia.
Askari hao wa Jeshi la Taifa la Ulinzi la Ethiopia (ENDF) wanaolinda uwanja wa ndege wa Bardale wamesema waliitungua ndege hiyo wakidhani kuwa ilikuwa mikononi mwa magaidi waliokuwa na lengo la kuiangusha katika angatua hiyo ndogo.
Ripoti ya awali ya uchunguzi wa tukio hilo imewanukuu askari hao ambao wanasisitiza kuwa hawakuwa na taarifa yoyote kuwa kulikuwa na ndege ndogo ya kiraia iliyotazamiwa kutua katika uwanja huo wa ndege.
Hata hivyo imebainika kuwa, askari hao wa Ethiopia waliotungua ndege hiyo kwa roketi Jumatatu iliyopita si miongoni mwa wenzao waliopo chini ya mwavuli wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM.
Ndege hiyo ya binafsi ilikuwa imebeba misaada ya kibinadamu inayohusiana na janga la corona wakati ilipoanguka ikikaribia kutua katika uwanja wa ndege wa Wilaya ya Bardale kusini mwa Somalia, yapata kilomita 300 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Katika tukio hilo, marubani wawili raia wa Kenya walipoteza maisha pamoja na raia wengine wanne wa Somalia. Ndege hiyo binafsi ni ya shirika la African Express Airways yenye makao makuu yake katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi