Sharti la Uturuki kukubali usitishaji vita nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61754-sharti_la_uturuki_kukubali_usitishaji_vita_nchini_libya
Ibrahim Kalin, Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Uturuki amesema kuwa usitishaji vita utatekelezwa nchini Libya kwa sharti kuwa wapiganaji wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Hafta waondoke katika mji wa Sirte.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 22, 2020 09:22 UTC
  • Sharti la Uturuki kukubali usitishaji vita nchini Libya

Ibrahim Kalin, Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Uturuki amesema kuwa usitishaji vita utatekelezwa nchini Libya kwa sharti kuwa wapiganaji wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Hafta waondoke katika mji wa Sirte.

Akizungumza karibuni na shirika la habari la France Press, Ibrahim Kalin amesema: Uturuki inaunga mkono takwa la Serikali ya Muafaka wa Kitaifa nchini Libya GNA la udharura wa kurejea nyuma askari wa Haftar hadi kwenye mstari wa mwaka 2015.

Kalin pia ameituhumu Ufaransa kwa kufanya juhudi za kuvuruga usalama wa Libya na kusema: Uungaji mkono wa Ufaransa kwa Khalifa Haftar unahatarisha usalama wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO, Bahari ya Mediteranea, Afrika Kaskazini na hasa usalama wa Libya.

Suala la usitishaji vita Libya sio suala geni. Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, kila upande unaopata nguvu na nafasi nzuri ya kijeshi umekuwa ukitoa masharti kuhusiana na suala zima la usitishaji mapaigano nchini humo. Kwa mfano, mwezi Februari mwaka huu ambapo askari wa Haftar walianza kuushambulia uwanja wa ndege wa Tripoli, mji mkuu wa Libya, na kuimarisha nafasi yao ya kijeshi katika nchi hiyo, waliipa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez Farraj, na ambayo inadhibiti Tripoli na maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo, pamoja na waungaji mkono wake na hasa Uturuki, masharti mahumu ya usitishaji vita.

Ibrahim Kalin, Msemaji wa Ikulu ya Uturuki

Kwa kutilia maanani ukweli huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ameelezea matumaini ya kutekelezwa usitishaji vita hivi karibuni nchini Libya na kuitaka Russia imshawishi Haftar akubali masharti ya usitishaji vita. Baada ya askari wa Haftar kushindwa katika medani ya vita na kulazimika kurea nyuma hadi katika maeneo ya mashariki mwa Libya, sasa jeshi lililoshinda katika medani ya vita ndilo linaloutwisha upande ulioshindwa masharti ya usitishaji mapigano.

Nukta ya kuzingatiwa hapa ni misimamo inayochukuliwa na serikali ya Uturuki badala ya Serikali ya Maufaka wa Kitaifa ya Libya. Baada ya kutia saini mapatano na serikali ya Fayez Sarraj, ambayo inatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa na serikali nyingi za dunia, viongozi wa Ankara wamekuwa wakitoa misimamo rasmi kuhusiana na masuala ya Libya badala ya serikali ya Tripoli. Ni wazi kuwa kushiriki makundi ya kigaidi na wanamgambo wa wanaofungamana na Uturuki katika vita vya Libya, kama yalivyo makundi yanayofungamana na nchi zingine zinazoshiriki katika mzozo wa nchi hiyo, kumefanya hali ya mambo huko Libya kuwa ngumu zaidi. Kuwepo kwa wapiganaji, wanamgambo na makundi ya kigaidi  kutoka Syria na Turkmenistan katika jeshi la Uturuki huko Libya kumezikasirisha nchi nyingi za Kiarabu. Mwezi Machi mwaka huu gazeti la Uingereza la The Guardian liliandika hivi kuhusu suala hilo:

Hisia dhidi ya Uturuki zimeongezeka sana kutokana na uingiliaji wa nchi hiyo katika masuala ya ndani ya Libya na kuna uwezekano wa chuki na hisia hizo kuongezeka kwa maslahi ya Khalifa Haftar.

Waziri Mkuu Fayez Farraj wa Libya akiwa na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki

Licha ya mapigano ya ndani nchini Libya na nafasi muhimu ya Uturuki katika ushindi wa hivi karibuni wa jeshi la serikali ya Fayez Sarraj, hapana shaka kwamba Uturuki ingali ina matatizo mengine mengi ambayo yanaikabili nchini humo. Nchi nyingi za Magharibi zinaunga mkono na kuwapa kila aina ya msaada askari wa Haftar, kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Kwa mfano Ufaransa inaendelea kuongeza kila siku askari wake nchini Libya kwa maslahi ya Haftar. Katika upande wa pili Russia inaonyesha kutoridhishwa na uwepo wa kijeshi na kiuchumi wa Uturuki katika ardhi ya Libya. Ni kutokana na ukweli huo ndipo hivi karibuni viongozi wa Ankara wakawatumia ujumbe viongozi wa Washington wakiwataka washirikiane pamoja kuhusu suala la Libya. Kwa hakika viongozi wa Uturuki wana wasi wasi kwamba huenda wasiwe na ubavu wa kukabiliana na serikali za Magharibi na Russia nchini Libya. Ni kutokana na suala hilo ndipo askari wa Uturuki wakaimarisha nafasi yao kufuatia ushindi wa jeshi la serikali ya Fayez Farraj nchini humo.

Kwa ujumla tunapasa kusema kuwa Uturuki haiwezi kubakia milele katika radhi ya Libya, na hasa ikitiliwa maanani kuwa kwa upande mmoja ina maadui sugu kama Imarati, Saudi Arabia na Misri na kwa upande wa pili sehemu kubwa ya Ulaya inapinga harakati za Uturuki nchini Libya.