Wahajiri 16 wafariki dunia baada ya boti yao kughariki pwani ya Libya
Watu wasiopungua 16 wamefariki dunia katika Bahari ya Mediterania baada ya boti yao kuzama, huko pwani ya Libya.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) liliripoti habari hiyo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, boti hiyo hafifu iliyozama huku ikiwa imebeba idadi kubwa ya wahajiri kupita kiasi, ilikuwa imetokea mji wa Zliten ulioko mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Wavuvi wa Libya wamesema walifanikiwa kuwanusuru watu 22 katika ajali hiyo ya Alkhamisi, wakiwemo raia wa Misri, Bangladesh, Syria, Somalia na Ghana na kwamba miongoni mwa watu 16 walioaga dunia ni mwanamme na mwanamke wa Syria.
Masoud Abdal Samad, afisa wa Gadi ya Pwani ya Libya amesema boti nyingi zilizobeba wahajiri hususan wa Kiafrika zinaondoka nchi humo karibu kila siku zikielekea Ulaya, lakini aghalabu yazo zinazama baharini kutoka na upepo mkali wakati huu wa msimu wa mapukutiko.
Mwezi uliopita wa Agosti, wahamiaji wasiopungua 45 kutoka nchi za Afrika walifariki dunia katika Bahari ya Mediterania kwenye ajali mbaya zaidi ya baharini kutokea katika pwani ya Libya katika mwaka huu wa 2020.
Ajali hiyo ilitokea wiki chache baada ya wahajiri wengine 40 kufariki dunia baada ya boti yao iliyokuwa njiani kuelekea Uhispania kughariki katika maji ya pwani ya Mauritania.
Mgogoro mkubwa wa wahajiri unaozizonga nchi za Ulaya umesababishwa na sera mbaya za nchi za Magharibi katika maeneo mbalimbali ya dunia hususan Asia Magharibi na vilevile umaskini mkubwa na ukosefu wa usalama katika baadhi ya nchi za Afrika.