Nigeria yaitaka Uingereza irudishe mali za nchi hiyo zilizoibiwa
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amesema ameitaka Uingereza izirudishe mali za nchi hiyo zilizoibwa na baadhi ya maafisa wa serikali na kupelekwa nchini humo.
Buhari amesema hatarajii kuombwa radhi na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ambaye ameitaja Nigeria "nchi yenye ufisadi wa kustaajabisha" lakini ameitaka nchi hiyo iziridushe mali walizoiba baadhi ya maafisa wa serikali ya Nigeria na kuzipeleka Uingereza.
Rais wa Nigeria ambaye yuko Uingereza kushiriki mkutano wa kupambana na ufisadi amesema, hamtaki yeyote amwombe radhi kwa sababu hakuna faida yoyote, lakini anataka Uingereza izirudishe mali za nchi yake.
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron leo anatazamiwa kuongoza mkutano wa kupambana na ufisadi utakaohudhuriwa pia na Marais Muhammadu Buhari wa Nigeria na Ashraf Ghani wa Afghanistan.
Siku ya Jumanne Cameron alinaswa katika picha ya video akimweleza Malkia Elizabeth wa nchi hiyo kuwa viongozi wa baadhi ya "nchi zenye ufisadi wa kustaajabisha" ikiwemo Nigeria na Afghanistan wanatazamiwa kuhudhuria mkutano wa kupambana na ufisadi utakaofanyika nchini humo.
Buhari ambaye mwaka uliopita alichaguliwa kuwa rais wa Nigeria, ameanzisha kampeni kubwa ya kupambana na ufisadi katika nchi hiyo.../