Somalia yadai jeshi la Kenya linaua raia katika hujuma zake za anga
Serikali ya Somalia kwa mara nyingine tena imekosoa vikali kile ilichodai kuwa ni tabia ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kuua raia wa Kisomali katika mashambulizi yake ya anga katika eneo la Gedo, jimbo la Jubaland kusini mwa Somalia.
Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imeashiria operesheni ya hivi karibuni ya KDF katika eneo la Gedo na kusisitiza kuwa, raia kadhaa wa Kisomali waliuawa katika hujuma za anga zilizofanywa na wanajeshi hao wa Kenya mnamo Juni 3.
Taarifa hiyo imesema jeshi la Kenya lilifanya mashambulizi ya anga ya kiholela dhidi ya miji ya El-Adde na Hisa-u-gur kwa madai ya kuyalenga maficho ya wanamgambo wa al-Shabaab, lakini yaliishia kuua raia wasio na hatia.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imesema itawasilisha malalamiko rasmi kwa Umoja wa Afrika, ikidai kuwa Kenya imekiuka makubaliano yanatoa miongozo kwa operesheni za Kikosi cha Kulinda Amani cha umoja huo nchini Somalia (Amisom).
Kenya ina askari karibu 3,500 wanaofanya kazi chini ya mwavuli wa Amisom nchini Somalia. Kenya haijatoa taarifa kuhusu madai hayo ya Somalia, kama ambavyo haijawahi kutoa taarifa kuhusu tuhuma za namna hii nchini Somalia huko nyuma.
Ikumbukwe kuwa, wanajeshi kati ya 180 hadi 200 wa Kenya waliokuwa chini ya mwavuli wa Amisom waliuawa katika shambulio la wanamgambo wa al-Shabaab katika kijiji cha El-Adde katika eneo hilo la Gedo, Januari mwaka 2016.