Maelfu waandamana kumuunga mkono Rais wa Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i75382-maelfu_waandamana_kumuunga_mkono_rais_wa_tunisia
Zaidi ya watu elfu tano wameshiriki maandamano ya kumuunga mkono Rais Kais Saied wa Tunisia anayetuhumiwa na upinzani kuhodhi madaraka yote ya utendaji ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 04, 2021 08:06 UTC
  • Maelfu waandamana kumuunga mkono Rais wa Tunisia

Zaidi ya watu elfu tano wameshiriki maandamano ya kumuunga mkono Rais Kais Saied wa Tunisia anayetuhumiwa na upinzani kuhodhi madaraka yote ya utendaji ya nchi hiyo.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, waandamanaji zaidi ya elfu tatu wameshiriki maandamano hayo katika mjii mkuu Tunis pekee, ikiwa idadi kubwa zaidi ya iliyojitokeza wiki iliyopita kupinga hatua zinazochukuliwa na rais huyo.

Baadhi ya watu wamesikika wakisema katika maandamanao hayo ya jana Jumapili kuwa, "Sisi sote ni Kais Saied, sisi sote ni Tunisia."

Kadhalika waadamanaji hao wamesikika wakitoa mwito wa kuvunjwa Bunge la nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Watu zaidi elfu moja wameshiriki maandamano kama hayo katika mji wa kiviwanda wa Sfax, huku idadi kama hiyo ikishiriki pia katika mji wa Sousse.

Maandamano katika mji mkuu wa Tunisia, Tunis

Tarehe 26 Julai, Rais Kais Saied alimuuzulu Waziri Mkuu Hichem Mechichi na kulisimamisha pia bunge la nchi hiyo. Sambamba na hatua hiyo, aliwaondolea wabunge kinga ya kisheria.

Kufuatia mwito uliotolewa wa kuanzisha tena shughuli za bunge, makumi ya wabunge Ijumaa iliyopita walielekea bungeni, lakini vikosi vya usalama viliweka ulinzi mkali na kuwazuia wabunge hao kuingia bungeni.