Umoja wa Mataifa waunga mkono kufanyika uchaguzi wa Libya katika wakati mwafaka
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amehimiza kufanyika uchaguzi mkuu wa Bunge na Rais katika tarehe mwafaka nchini Libya.
António Guterres ametoa mwito huo usiku wa kuamkia Ijumaa ya leo na huku akigusia tangazo la tarehe 22 Disemba la Tume Kuu ya Uchaguzi ya Libya la kuakhirisha uchaguzi huo na kutangazwa tarehe mpya ya kufanyika kwake, amesema, uchaguzi wa Rais na Bunge la Libya unapaswa kufanyika katika wakati unaofaa kwa lengo la kuhakikisha makabidhiano ya madaraka yanafanyika kwa amani na kwa njia ya kidemokrasia.
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameipongeza pia Tume Kuu ya Taifa ya Uchaguzi ya Libya kwa kulihimiza bunge la nchi hiyo kuhakikisha linarahisisha mchakato wa kufanyika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo katika wakati unaofaa. Tume hiyo ya uchaguzi ya Libya imependekeza kuakhirishwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo kutoka tarehe 24 mwezi huu wa Disemba yaani leo hadi mwezi Februari 2022 baada ya kufanyika maandamano mbele ya jengo la tume hiyo ya watu wanaolalamika kwamba hivi sasa mazingira mazuri hayajaandaliwa ya kufanyika uchaguzi kama huo.
Sababu ya kushindwa kufanyika uchaguzi huo leo kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali imetajwa kuwa ni kutotolewa orodha ya mwisho ya majina ya wagombea, kutopatikana kibali cha kuanza kampeni za uchaguzi na kuweko matatizo ya kimahakama kutokana na mashtaka dhidi ya wagombea.
Malik Traina mwana habari wa Kanali ya Televisheni ya al-Jazeera anasema kuwa: Katika hali ambayo katika majuma ya hivi karibuni kulikuwa na uwezekano wa kuakhirishwa uchaguzi wa Libya, kulikuweko na hitilafu baina ya Tume Kuu ya Uchaguzi na Kamati ya Bunge juu ya nani anapaswa kubeba jukumu la tangazo la kuakhirishwa uchaguzi hhuo. Inaelezwa kuwa, Kamati Kuu ya Uchaguzi ilikuwa imetangaza wazi na bayana kwamba, Bunge ndilo linalopaswa kuzungumzia suala la tarehe mpya ya kufanyika uchaguzi huo.
Kuna mitazamo miwili nchini Libya kuhusiana na uchaguzi ambao imeshikana kufanyika leo. Kundi moja lilikuwa likisisitiza juu ya kufanyika uchaguzi katika tarehe iliyokuwa imepangwa likiamini kwamba, hatua hiyo itapelekea kupatikana mshikamano wa kitaifa na hivyo kutosambaratika matunda ya kisiasa na kiusalama yaliyopatikana. Kundi la pili lilikuwa likiashiria matatizo na mapungufu ya kisheria, kimahakama na miundombinu na linaamini kwamba, kwa kuzingatia matatizo na mapungufu haya yaliyopo, kufanya uchaguzi katika mazingira haya kunaweza kuitumbukiza Libya katika kinamasi cha vita vya ndani.
Mintarafu hiyo, kadiri siku za kufanyika uchaguzi huo wa Bunge na Rais zilivyokuwa zikikaribia ndivyo kulivyokuwa kukishuhudiwa mizozo na mivutano zaidi. Masuala kama kufanyika au kutofanyika uchaguzi, namna ya kuendesha zoezi lenyewe, kuanishah vituo vya kupigia kura na kufahamika majina ya wagombea ni miongoni mwa zilizokuwa changamoto kuu kuhusiana na uchaguzi wa Libya ambao sasa umeakhirishwa.
Kimsingi ni kuwa, licha ya mazunguzmo yote yaliyofanyika na hata juhudi za kisiasa zilizofanyika kieneo na kimataifa, lakini anga ya kisiasa ya Libya inakabiliwa na changamoto mbili kuu yaani kuendelea hitilafu na mivutano ya ndani na kuongezeka uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Hatupaswi kuacha kusema pia kuwa, baadhi ya madola ya Magharibi kama Uingereza na Marekani yalikuwa yakitaka uchaguzi wa Libya uakhirishwe.
Katika upande mmoja, hitilafu kuhusiana na tarehe iliyoainishwa hapo kabla ya kufanyika uchaguzi huo yaani leo, zilipamba moto baada ya Mahakama ya Rufaa kubatilisha hatua ya mahakama za awali za kuwazuia kushiriki katika uchaguzi huo, Seif al-Islam Gaddafi na Khalifa Haftar waliotangaza nia ya kugombea kiti cha urais, na katika upande wa pili kuliibuka wasiwasi wa kushtadi harakati za madola ya kigeni katika nchi hiyo. Hali hii iliifanya serikali ya muda wa Libya kukabiliwa na changamoto na kibarua kigumu.
Siku chache zilizopita na baada ya wapinzani kukusanyika mbele ya makao makuu ya Tume Kuu ya Uchaguzi wakilalamikia mwendo wa kinyonga wa mchakato wa uchaguzi huo, tume hiyo ikapendekeza kuwa, uchaguzi huo uakhirishwe hadi tarehe 22 Januari mwakani kutokana na kuendeleza hitilafu na mivutano baina ya washindani wa ndani na wa nje kuhusiana na uchaguzi huo.
Hapana shaka kuwa, uakhirishwaji wa uchaguzi wa Libya ambao umefanyika baada ya miezi kadhaa ya mashinikizo ya kufanyika uchaguzi huo yaliyoambatana na mazungumzo ya ndani na ya kimataifa, ni pigo kwa juhudi zenye lengo la kuboreshha hali mbaya ya mambo nchini humo iliyodumu Libya kwa miaka 10 sasa tangu aondolewe madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi.