Odinga aenda mahakamani kupinga matokeo ya urais Kenya
Mgombea urais wa Kenya kwa tiketi ya chama cha Muungano wa Azimio la Umoja wa One Kenya, Raila Odinga amewasilisha mahakamani shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC hivi karibuni.
Odinga ameongozana na mgombea mwenza, Martha Karua, na vigogo wengine wa muungano huo akiwemo Kalonzo Musyoka na chama cha Wiper, na Gideon Moi wa chama cha KANU.
Mawakili wa Odinga wakiongozwa na Gavana mteule wa Siaya, James Orengo wamewasilisha makasha 39 yenye vithibiti na nyaraka wanazosema zina ushahidi wa kuonesha kuwa uchaguzi wa Agosti 9 ulikumbwa na udanganyifu, mizengwe na kasoro nyingi.
Majaji saba wa Mahakama ya Juu wanatazamiwa kulisikiliza shauri hilo na kutoa uamuzi ndani ya siku 14 zijazo; na sasa mchuano mkali baina ya mawakili waandamizi wa upande wa Odinga, IEBC na timu ya Naibu Rais, William Ruto unatazamiwa kushuhidiwa mahakamani hapo.
Wiki iliyopita, mwanasiasa huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 77 alisema hakubaliani na matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyotangazwa na IEBC, kwa sababu mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alikiuka katiba kabla ya kumtangaza mshindi.
Amesema makamishna wa tume hiyo hawakukubaliana kuhusu hesabu ya mwisho ya matokeo hayo yaliyompatia ushindi mshindani wake mkuu William Ruto, aliyewania kwa chama cha UDA.
Makamishna wanne kati ya saba wa tume ya uchaguzi wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti, Juliana Cherera walijitenga na matokeo hayo yaliyotangazwa na Chebukati, wakidai kwamba marhala ya mwisho ya mchakato wa kuyatangaza haikuwa na uwazi.
IEBC ilimtangaza Ruto mshindi wa uchaguzi wa rais, kwa kuapata kura milioni 7.1, sawa na asilimia 50.49 ya kura milioni 14 zilizopigwa, huku Raila akiambulia kura milioni 6.9, sawa na asilimia 48.85 ya kura.